Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza awaandalia dozi nzito Yanga

Kocha Mkuu Wa Dodoma Jiji, Francis Baraza Francis Baraza

Sun, 4 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Dodoma Jiji kimetua jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaopigwa kesho Jumatatu, huku kocha mkuu Francis Baraza akiweka wazi wamejiandaa kiakili na kimwili kwa lengo la kuondoka na pointi zote tatu.

Timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 1:00 usiku huku Yanga ikitoka kulazimishwa suluhu juzi katika mchezo wa kusisimua dhidi ya Kagera Sugar uliopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baraza ambaye huo ni mchezo wa kwanza akiwa na kikosi hicho tangu atambulishwe Desemba 16, mwaka jana kuchukua nafasi ya Melis Medo aliweka wazi haitakuwa rahisi kwao ingawa wamejipanga vyema.

“Hautakuwa mchezo mwepesi kwa sababu unapokutana na timu kama Yanga ambayo ina wachezaji wazuri ni lazimaujiandae vizuri. Tunatambua ugumu ila maandalizi tuliyoyafanya kwa wiki zaidi ya tatu yametuimarisha,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Kagera Sugar aliongeza kuwa hali ya kikosi ni nzuri ingawa katika mchezo huo watamkosa beki wa kulia, Anderson Kimweri ambaye amepewa mapumziko maalumu kutokana na kupata msiba wa baba yake mzazi.

Mchezo wa mwisho kwa timu hizo uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Mei 13, mwaka jana Yanga ilishinda kwa mabao 4-2, huku mechi hiyo ikikumbukwa zaidi kwani ndio iliyoipa rasmi Yanga ubingwa wa 29 wa ligi hiyo tangu 1965 ikitetea taji kwa msimu wa pili mfululizo. Dodo Jiji ina alama 18 ilhali Yanga inazo 31.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: