Kutangazwa kwa Kocha Mkuu mpya wa Dodoma Jiji FC, Francis Baraza, kunatajwa kama sababu ya kukiongezea nguvu kikosi cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, imeelezwa.
Kocha Msaidizi wa Dodoma Jiji, Kassim Lyogope, amesema wanaamini Baraza ataisaidia timu hiyo kufikia malengo na muda wa kuijenga na kuimarisha timu bado upo.
Lyogope amesema pia yeye amefurahi kuungana na Kocha huyo kutoka nchini Kenya, kwa sababu anaamini atamwongezea mbinu za kufundisha kutokana na uzoefu ambao kocha huyo anao.
“Tutazaliwa upya, Dodoma Jiji itaimarika na itabadilika, tusubiri mambo mazuri baada ya ujio wa Baraza, anaijua Ligi Kuu ya Tanzania, anawajua wachezaji wengi wa hapa nchini, kikubwa ni tuongeze ushirikiano katika kutimiza majukumu yetu,” amesema kocha huyo.
Ameongeza wameshaanza kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika mechi zilizopita na wataingia kwenye mzunguko wa pili wakiwa na nguvu mpya.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Dodoma Jiji yenye alama 18 iko kwenye nafasi ya saba baada ya kucheza michezo 13 wakati vinara wa ligi hiyo ni Azam FC yenye alama 28 baada ya kushuka dimbani mara 12.