Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza amrithi Maxime Kagera

17c38dcded3e0d54f05caad39e1160df.jpeg Baraza amrithi Maxime Kagera

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Francis Baraza amesaini mkataba wa miaka miwili na nusu kuifundisha Kagera Sugar jana na kusema mazingira mazuri ndio yaliyomvutia kujiunga na Wanankurukumbi.

Baraza raia wa Kenya ambaye alikuwa akiifundisha Biashara United anachukua nafasi ya Mecky Maxime aliyefutwa kazi hivi karibuni. Akizingumza na gazeti hili kwa njia ya simu Baraza aliushukuru uongozi wa Biashara United kwa ushirikiano waliompa kwa kipindi chote alichoifundisha timu hiyo.

Alisema maslahi ya wachezaji na kocha ndio yaliyomvutia kujiunga na Kagera kwani yanamhakikishia mazingira mazuri ya kufanya kazi kwa utulivu na kutafuta changamoto mpya.

“Nashukuru nimesaini mkataba wa miaka miwili na nusu, kilichonivutia kujiunga na Kagera ni maslahi mazuri ya wachezaji pamoja na mimi kwani yananihakikishia kufanya kazi kwa utulivu,” alisema Baraza.

Baraza ambaye alijiunga na Biashara mwaka 2019 akitokea Chemelil Sugar FC aliikuta timu hiyo ikiwa katika hali mbaya na miongoni mwa timu zilizokuwa hatarini kushuka daraja msimu uliopita lakini aliweza kuibadili na ikanusurika na kuiwezesha kumaliza msimu wa 2019/2020 ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.

Lakini msimu huu ameendelea kudhihirisha ubora wake ambapo hadi sasa ameiongoza Biashara kuwepo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 39 baada ya kucheza michezo 23 na huenda ndicho kilichomfanya uongozi wa Kagera Sugar kumchukua.

Biashara imekuwa ikionesha ushindani inapocheza katika uwanja wa nyumbani au ugenini na imepoteza mechi nne tu ugenini hadi sasa na amefanikiwa kuinua viwango vya wachezaji kama Abdulmajid Mangalo, Lenny Kisu na Deogratias Judika kuwafanya wageuke lulu katika soko la usajili.

Ana kazi ya kuindoa Kagera Sugar katika nafasi ya 13 ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza michezo 24 kwani haipo sehemu salama na kuipandisha juu kukwepa kuangukia kucheza mtoano.

Baraza amewahi kuwa kocha mkuu wa Chemelil Sugar FC, Sony Sugar FC kocha msaidizi wa Tusker FC na timu za vijana za Muhoroni na Western Stima zote za Kenya.

Chanzo: www.habarileo.co.tz