Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza aanza na wavivu Kagera Sugar

Baraza Pic Data Baraza aanza na wavivu Kagera Sugar

Wed, 24 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza baada tu ya kutua ndani ya kikosi hicho alikaa kikao na wachezaji ikiwamo kuwapa masharti mapya, moja likiwa ni kukatwa mshahara kwa kila mchezaji atakayeonyesha utovu wa nidhamu ikiwemo kukosa mazoezi bila sababu ya msingi.

Baraza alijiunga na Kagera Sugar hivi karibuni kama kocha mkuu akitokea Biashara United ambayo ameiacha ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo raia wa Kenya alisema amegundua wachezaji wengi wa timu hiyo hawakuwa wakijitoa uwanjani na haraka alikaa nao kikao ili kupanga mambo mbalimbali yatakayoinyanyua na kuipeleka nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Baraza ana kazi kubwa ya kuibakiza Kagera Sugar kwenye ligi msimu ujao kwani timu hiyo iliyokuwa ikinolewa na Mecky Maxime iko nafasi ya 13 ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza michezo 24, kushinda sita, sare saba na kupoteza 11.

“Nimeanza majukumu yangu ndani ya timu tangu Jumatano iliyopita na jambo la kwanza nilipofika ni kukutana na viongozi pamoja na wachezaji ili kujuana na kuweka mambo sawa lakini baadaye nikakutana na wachezaji pekee ili tuyajenge na kupanga mikakati ya kuhakikisha timu inakuwa sehemu salama,” alisema.

“Kitu ambacho niligundua wakati naifuatilia timu hii ni wachezaji kutokuwa katika hali ya kujitoa uwanjani, morali yao ilikuwa chini na ndio maana nilivyofika tu nilikaa nao kikao ili kujua matatizo yao na jinsi gani tufanye ili kurudisha ubora wa timu.

“Kitu kikubwa nilichowaambia ni kila mchezaji kujitoa na kupenda mazoezi kwani najua wachezaji wengi wa Kitanzania ni wavivu wa mazoezi, yaani ingekuwa uwezo wao timu zingekuwa zinafanya mazoezi siku moja kisha zinapumzika siku mbili ndio zifanye tena.

“Sasa nimewaambia mimi sio kocha wa namna hiyo kwani napenda wachezaji wanaopenda mazoezi na kujibidisha uwanjani. Nimewapa masharti kuwa yule atakayekosa mazoezi bila sababu ya msingi atakatwa mshahara na pia hata yule atakayeonyesha utovu wa nidhamu, sitamvumilia.”

Baraza alisema utaratibu huo ndio aliokuwa akiutumia hata alipokuwa akiinoa Biashara United na ni sababu ya timu hiyo iko sehemu ilipo kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na kiwango bora. Biashara ni ya nne.

“Ukweli kikosi kina wachezaji wazuri wenye viwango bora, muhimu ni kurejesha morali yao.”

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz