Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baraza: Wachezaji wangu wamekosa vibali

KAGERA Sugar Head Coach Francis Baraza Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Francis Baraza

Wed, 14 Feb 2024 Chanzo: Dar24

Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC, Francis Baraza amesema sababu ya kushindwa kuwatumia nyota wake wawili wa kimataifa waliosajiliwa dirisha dogo katika mechi za Ligi Kuu Bara ni kukosa vibali.

Nyota hao ni Robinson Kamura kutoka Kakamega Home Boys na kiungo Apollo Onyango kutoka KCB zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Kenya (FKF PL) na walishindwa kuonekana katika mechi mbili dhidi ya Young Africans na Mashujaa FC.

Baraza amesema uongozi wa timu unashughulikia ili vipatikane kwa haraka na waweze kuongeza nguvu kwenye kikosi.

Amesema kama taratibu za kupata vibali zitakamilika mapema, huenda wachezaji hao akawatumia katika mchezo dhidi ya Coastal Union FC, kesho Alhamis (Februari 15) kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.

“Wengi walijua labda ni majeruhi, lakini niwatoe tu wasiwasi nyota wetu ni wazima wa afya na uongozi unapambana ili kupata vibali waanze kutumika,” amesema Baraza.

Ametumia fursa hiyo kuzungumzia maandalizi ya mchezo wa kesho Alhamis (Februari 15) dhidi ya Coastal Union FC na amesema licha ya kusafiri kwa umbali mrefu lakini anaamini watapata ushindi kutokana na jinsi walivyojiandaa.

Baraza ambaye amewahi kuzifundisha timu za Biashara United, Kagera Sugar za Tanzania Bara, pia Polisi na Awendo Sony Sugar za nchini kwao Kenya aliweka wazi mchezo dhidi ya Coastal utakuwa mgumu sana ukizingatia timu zote zimetoka kulazimishwa sare.

Tuko vizuri na naamini tutapata matokeo mazuri kutokana na rekodi yetu nzuri dhidi ya Coastal tunapokutana, lakini kikubwa ni wachezaji wangu kutumia vyema nafasi ambazo tutatengeneza,” amesema Baraza.

Chanzo: Dar24