Ligi Kuu Bara imekusanya mastaa kibao wa kimataifa kutoka nje ya Tanzania ambao baadhi yao wamebahatika kuitwa katika vikosi vya timu za taifa za nchi zao ambazo wikiendi hii zimefuzu ushiriki wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) za mwaka 2023 zitakazofanyika mwakani huko, Ivory Coast.
Achana na nyota wazawa wa Tanzania walioipigania Taifa Stars na kuipeleka fainali zijazo za Afcon 2023 ikiwa ni mara ya tatu baada ya zile za kwanza za 1980 huko Nigeria na zile za 2019 zilizofanyika Misri, hapa ni mastaa wa Ligi Kuu Bara kutoka mataifa ya nje ambao wamezishuhudia timu zao zikienda Ivory Coast wakiwa na vikosi hivyo.
Kuna wale waliozichezea timu za mataifa yao kwenye mechi za awali za makundi za kuwania tiketi hiyo ya Ivory Coast, lakini bahati mbaya kwao hawakuitwa na kuwaacha mastaa watano tu wa kigeni wanaoungana na wazawa kutoka Tanzania wanaocheza Ligi Kuu Bara kwenda kwenye fainali hizo za Afcon.
Wakati mastaa hao wakihitimisha mchakato huo mastaa wengine wanne bado wana kibarua kuipambania timu yao kupata ushiriki kwenye mashindano hayo si wengine ni Said Ntibazonkiza ‘Saido’, kipa Justin Ndikumana, Jonathan Nahimana na Derrick Mukombozi.
Wanne hao wanatarajia kushuka uwanjani leo Jumanne kuipigania Burundi ipate nafasi ya kufuzu kushiriki fainali za mataifa ya Afrika wakiwa kundi C kwa kuvaana na Cameroon ugenini. Kundi hilo lina timu tatu baada ya Kenya kufungiwa na Fifa.
Timu hizo ni Namibia ambayo tayari imefuzu kucheza fainali zijazo kutokana na matokeo bora dhidi ya wapinzani wake, Cameroon na Burundi zenyewe zote zina pointi nne na leo zitacheza mechi ambayo itaamua nani aungane na mataifa mengine kucheza fainali za AFCON.
Mwanaspoti linakuletea mastaa watano ambao tayari wamezihakikishia timu zao za taifa kucheza fainali hizo mapema mwaka huu.
DJIGUI DIARRA
Ni kipa namba moja wa Yanga, ambaye tangu ametua kwenye kikosi hicho ameisaidia timu yake kutwaa mataji sita akichukua Ngao ya Jamii, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ligi Kuu Bara yote mara mbili mfululizo.
Ubora wake akiwa Tanzania umeonekana pia kimataifa akiiongoza timu ya taifa ya Mali iliyokuwa Kundi G kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Sudan Kusini akicheza dakika zote 90 na kuipeleka timu katika fainali hizo kwa kufikisha jumla ya pointi 15.
Tangu Diarra amejiunga na mabingwa watetezi wa ligi, Yanga, kiwango chake kimezidi kuimarika akishinda tuzo mbalimbali kama kipa bora wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kipa bora wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo.
HENOCK INONGA
Beki wa kati aliye mhimili wa ukuta wa kikosi cha kwanza cha Simba, alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliokuwapo wakati timu ya taifa ya DR Congo ikikata tiketi ya Afcon 2023 wakati wakiifumua Sudan kwa mabao 2-0 jijini Kinshasa licha ya kuchelewa kujiunga kikosini kutokana na kujitibia majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.
Inonga, ambaye ni panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Simba chini ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, aliumia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Singida Big Stars na hajapata nafasi ya kuichezea timu yake katika mechi mbili za Ligi Kuu lakini jina lake lilikuwapo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo.
Licha ya kutopata nafasi ya kucheza ameandika historia ya kuwa miongoni mwa mastaa walioitwa kuitumikia timu hiyo ambayo imeongoza msimamo wa Kundi I ikiwa na pointi 12. Katika mchezo huo nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele alitokea benchini na kufunga bao la pili baada ya awali nyota wa Spartak Moscow, Theo Bongonda kuitanguliza mapema kipindi cha kwanza.
STEPHANE AZIZ KI
Alijiunga na Yanga msimu uliopita na hakuwa na ubora sana kwenye nafasi aliyokuwa akicheza sambamba na mzawa Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye ametimkia Azam FC. Msimu huu amerudi upya na kuonyesha ushindani ndani ya kikosi cha Yanga.
Kiungo-mshambuliaji huyo ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Burkina Faso ambayo ilikuwa kundi B, ameiwezesha kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023).
Ki aliingia kipindi cha pili kuipambania timu yake kupata nafasi hiyo ambayo mchezo ulimalizika kwa suluhu dhidi ya Eswatini na kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi B baada ya kukusanya pointi 11 ikiitangulia Cape Verde iliyomaliza ya pili na kusonga nayo kwenda Ivory Coast.
CLATOUS CHAMA
Kiungo fundi wa mpira wa Simba alikuwa kwenye orodha ya mastaa walioitwa kuitumikia timu yao ya taifa ya Zambia ambayo ilikuwa kundi H ikifuzu kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) kwa kuongoza kundi hilo kwa pointi 13 Chama hakupata nafasi ya kucheza alikaa benchi timu yake ikiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Comoros.
Chama ambaye ameanza vyema msimu huu akiifungia timu yake bao moja kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara, alikuwa miongoni mwa wachezaji walioitwa na Chipolopolo.
Zambia imefuzu mapema kutoka kundi H ikiwa kinara mbele ya wenyeji wa fainali zijazo, Ivory Coast, huku Chama akiwa benchi kwenye mchezo wa mwisho, akimfunika Kennedy Musonda wa Yanga ambaye safari hii hakuitwa kwenye kikosi hicho, licha ya awali kuitumikia kwenye mechi za mwanzoni.
CHEIKH SIDIBE
Huyu ni beki wa kushoto wa Azam FC aliyesajiliwa katika dirisha kubwa lililofungwa Agosti 31 akiitumikia timu hiyo kwa mechi mbili tu za Ligi Kuu Bara na nyingine za Kombe la Shirikisho Afrika ambako walitolewa katika hatua ya kwanza kwa penati 4-3 kufuatia matokeo ya jumla kuwa sare ya 3-3 dhidi ya Bahir.
Beki huyo mahiri alikuwa miongoni mwa mastaa walioitwa kuitumikia timu yao ya taifa ya Senegal ambayo tayari umefuzu ushiriki wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2023) ikiwa kundi L na imemaliza nafasi ya kwanza kwa pointi 14.
Sidibe ndiye aliyetoa pasi kwa mfungaji wa bao la kuongoza la Senegal, Lamine Camara kiungo anayekipiga (Metz ya Ligi Kuu ya Ufaransa) kabla ya Rwanda kulichomoa.