Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) mzunguko wa kwanza umekamilika leo katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma kwa timu ya Baobab Queens kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya The Tiger ya Jijini Arusha.
Mabao ya Baobab yamefungwa kipindi cha kwanza na Jamila Rajabu dakika za 16 na 28. Licha ya Baobab kuibuka na ushindi, kiungo wa The Tiger Samantha Okeya alionesha uwezo mkubwa na kuwapoteza viungo wa Baobab Queens,Zuhura Sahabu na Halima Mwangomole
Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu
Huu ni mchezo wa kiporo ambao ulitakiwa kufanyika Januari 5 mwaka huu,lakini uliahirishwa kutokana na The Tiger kutotokea uwanjani.
Huu ni ushindi wa tatu kwa Baobab Queens msimu huu katika michezo tisa iliyocheza,imepoteza minne,imetoa sare miwili.
The Tiger imepoteza michezo saba, imeshinda mmoja,sare mmoja,imefungwa mabao 25,imefunga sita,ina pointi nne,kwenye msimamo wenye timu 10 inashika nafasi ya nane.
Katika mabao 10 yaliyofungwa na Baobab Queens matano yamefungwa na Jamila Rajabu.
Anaeongoza kwa kufunga mpaka sasa ni Oppa Clement wa Simba Queens mwenye mabao tisa akifuatiwa na Jentrix Shikangwa nae wa Simba Queens mwenye mabao saba na Winfrida Charles wa Alliance Girls anashika nafasi ya tatu akiwa na mabao sita.
Jamila Rajabu,Neema Charles,Martha John na Zuhura wa Baobab Queens wameanza katika michezo yote tisa ya mzunguko wa kwanza WPL.
The Tiger inashika nafasi ya pili kwa kufungwa mabao mengi,imefungwa mabao 25,Amani Queens ndio kinara imefungwa mabao 28,Simba Queens inaongoza kwa kufunga mabao mengi imefunga 29 ikifuatiwa na JKT Queens mabao 23,Fountain Gate Princess mabao 21.