Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bao la Mzambia lamkuna kocha Coastal

X Casc Shedrack Mulungwe

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mkenya David Ouma amesifu kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, Shedrack Mulungwe raia wa Zambia wakati kikosi hicho kilipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 jana kikiwa ugenini mjini Kigoma mbele ya wenyeji Mashujaa.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Mulungwe alicheza mechi ya kwanza tangu atue nchini akitokea Nkwazi FC na kufunga bao la kwanza, huku lile la ushindi likifungwa na Bakari Selemani aliyerejea baada ya kutoka majeruhi.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo huo, Ouma amesema ni jambo jema kwa nyota huyo kucheza mechi ya kwanza na kufunga kwani hakuwa na papara ya kumtumia haraka kwa sababu alihitaji apone vizuri jeraha lake lililokuwa linamsumbua.

"Mulungwe tulimsajili tangu dirisha kubwa, lakini kutokana na majeraha ya goti tuliamua kumtoa katika mfumo wa usajili ili kumuuguza, Januari mwaka huu ndipo tukamrudisha na kwa hakika tumeanza kuona matunda yake," amesema Ouma.

Ouma ameongeza, lengo la timu hiyo kwa sasa ni kuendelea kupambania moja ya nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu, kwani uwezo huo kwa sasa wanao kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa na mwenendo mzuri wa matokeo katika mechi zao za nyumbani na za ugenini.

Mchezo huo ulikuwa wa 22 msimu huu kwa Coastal katika Ligi Kuu ikishinda tisa, sare sita na kupoteza saba ikiwa nafasi ya nne na pointi 33, ikisaliwa na michezo minane kabla ya kukamilisha msimu, ilihali kileleni Yanga bado inaongoza kwa pointi 52 ikicheza mechi 20, huku Azam na Simba zikifuata nyuma ya watetezi hao.

Ushindi huo ni wa pili msimu huu kwa Coastal dhidi ya Mashujaa, kwani mechi ya mzunguko wa kwanza zilipokutana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga Oktoba 25 mwaka jana, Wagosi wa Kaya walishinda kwa mabao 2-0 yakifungwa na Bakari Seleman na Lucas Kikoti.

Chanzo: Mwanaspoti