Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bao bora Qatar 2022 atafunga nani?

Richarlison Goal Richarlison alifunga moja ya mabao makali

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Lipi lile la Richarlison? Au lile la Gavi dhidi ya Costa Rica? Au lile la Vincent Aboubakar alilowafunga Serbia?

Ni mjadala wa bao bora la fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

Tuzo ya Bao Bora la Fainali za Kombe la Dunia ilianza kutolewa 2006, ambapo mashabiki wamekuwa wakipiga kura na kuchagua bao moja ambalo wanadhani lilifungwa kwa ustadi mkubwa ni bora kwa michuano hiyo.

Kwa maana hiyo, fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar zitashuhudia mchezaji wa tano kuchukua tuzo ya Bao Bora la michuano baada ya kushuhudia wakali wanne tayari wakinyakua tuzo hiyo.

Supastaa wa Argentina, Maxi Rodriguez ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kubeba tuzo hiyo baada ya kuanzishwa kwake kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006 huko Ujerumani, ambapo bao alilofunga dhidi ya Mexico katika mechi ya hatua ya 16 bora huko Lepizig ndilo lililochaguliwa kuwa bora.

Wakati ikisubiriwa kuona ni nani atabeba tuzo hiyo ya Bao Bora la fainali za Kombe la Dunia 2022, hawa hapa mastaa ambao walifunga mabao ya viwango na kunyakua tuzo ya bao moja kwenye fainali hizo za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Benjamin Pavard: Ufaransa v Argentina (2018)

Wakati inapenyapenya kwenda kubeba ubingwa wa dunia huko Russia 2018, Ufaransa iliichapa Argentina katika mechi ya hatua ya 16 bora kwenye Uwanja wa Kazan Arena na siku hiyo kulishuhudiwa bao matata kabisa la beki Benjamin Pavard, ambalo baadaye lilichaguliwa kuwa bora kwenye fainali hizo. Pavard alifunga kwa shuti kali sana kuisaidia Ufaransa kushinda 4-3 na kupata tiketi ya kwenda kuwakabili Ubelgiji robo fainali kabla ya kuwachapa Croatia mabao 4-2 kwenye fainali.

James Rodriguez: Colombia v Uruguay (2014)

Fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil zilikuwa bora kabisa kwa James Rodriguez, ambapo alifunga mabao sita na kunyakua Kiatu cha Dhahabu.

Kwenye mabao yake hayo, staa huyo wa Colombia, bao lake alilowafunga Uruguay kwenye hatua ya 16 bora lilikuwa tamu kwelikweli na kumfanya ashinde tuzo ya Bao Bora la fainali hizo za Brazil 2014.

Rodriguez alipokea pasi ya mpira wa kichwa nje ya boksi na kutuliza kifuani kabla ya kupiga shuti kali kutikisa nyavu.

Diego Forlan: Uruguay v Ujerumani (2010)

Diego Forlan aliitumikia Uruguay kwenye fainali tatu za Kombe la Dunia (2002, 2010 na 2014), lakini fainali za Afrika Kusini 2010 alikuwa kwenye wakati mzuri zaidi.

Hakika mpira wa Jabulani ulipendezana na miguu yake, ambapo alikuwa akifunga mabao makali kwelikweli likiwamo lile alilowafunga Ujerumani, lililochaguliwa kuwa bao bora la michuano.

Forlan alimaliza michuano hiyo akiwa kinara wa mabao baada ya kufunga mara tatu. Uruguay ilitolewa na Uholanzi katika nusu fainali.

Maxi Rodriguez: Argentina v Mexico (2006)

Akienda kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006 huko Ujerumani, Maxi Rodriguez tayari alikuwa amejishajitengenezea jina kama mchezaji muhimu kwenye kiungo ya Argentina. Mzaliwa huyo wa Rosario alitumiwa kwenye mechi zote tatu za hatua ya makundi na kocha Jose Pekerman na kwenye mechi ya Serbia&Montenegro alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 6-0. Waliongoza kundi na kwenda kuwavaa Mexico kwenye hatua ya 16 bora, ndipo Rodriguez alipofunga bao la mashindano.

Chanzo: Mwanaspoti