Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Banka anukia Ruvu Shooting

Mo Banke.jpeg Banka anukia Ruvu Shooting

Tue, 27 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo, Mohammed Issa ‘Banka’ yuko kwenye mazungumzo na viongozi wa Ruvu Shooting ili kujiunga nao katika dirisha hili dogo.

Banka ameamua kuvunja mkataba wake uliosalia na timu yake ya Namungo kwa malengo ya kutafuta changamoto mpya huku suala la kutolipwa stahiki zake kwa wakati zikielezwa kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha nyota huyo kuondoka timu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zilitonya kwamba ni kweli staa huyo amefanya mazungumzo na kocha wa kikosi hicho, Mbwana Makata na endapo atamridhia basi atapewa dili la miezi sita kumalizia msimu.

“Timu yetu haiko kwenye wakati mzuri, hivyo tunahitaji kupata wachezaji wazoefu ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo watakaotutoa huku chini tulipo kwani hata mashabiki wetu hawafurahishwi na mwenendo wetu,” kilisema chanzo chetu.

Kwa upande wa ofisa habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Masau Bwire alisema wanaendelea kupitia ripoti ya kocha wao mkuu, Mbwana Makata na wachezaji ambao watafikia makubaliano nao ili kuwatumikia watawaweka wazi.

“Kwenye dirisha hili ni lazima tuwe makini sana kwa sababu tunataka wachezaji ambao watakuja moja kwa moja kwenye kikosi chetu na kucheza, hatutaki tumtoe mtu huko aliko aje hapa akae tena benchi,” alisema Masau.

Endapo dili hilo litakamilika utakuwa ni usajili wa pili kwenye dirisha hili kwa Maafande hao baada ya awali kumsainisha mshambuliaji wa zamani wa Biashara United, Atupele Green aliyekuwa anaichezea Kyetume ya Uganda.

Ruvu Shooting inapamba ili kuweza kujinasua kwenye nafasi za chini katika Ligi Kuu.

Chanzo: Mwanaspoti