Kikosi cha Yanga kinashuka uwanja wa nyumbani leo Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku kucheza mechi ya pili ya Kundi D ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, lakini kuna mastaa wao wawili wameliamsha huko kambini jana.
Yanga itaikaribisha TP Mazembe ikiwa imetoka kupoteza mchezo wa kwanza ugenini mbele ya US Monastir na katika kuhakikisha mechi hiyo ya pili katika kundi hilo na ya kwanza nyumbani msimu huu inaenda sawa, Mchezaji Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Yannick Bangala katika hali isiyotarajiwa jana alisimamisha mazoezi kisha kutoa darasa kwa wenzake.
Katika maneno yake Bangala alisema; “Sikilizeni ndugu zangu, tunakwenda kucheza mechi kubwa sana tangu nifike hapa Yanga, hii ni mechi ambayo itakuwa na heshima kubwa kama Wanayanga, lakini kwa sisi Wakongomani tuliopo hapa ni kubwa zaidi kwa kuwa ni mechi ya watani, tukafanye kweli.”
Kauli ya Bangala ilikuwa inamaanisha Yanga ina wachezaji sita kutoka DR Congo ambao ni yeye mwenyewe, Fiston Mayele, Tuisila Kisinda, Jesus Moloko, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa ambao wote wameitumikia AS Vita Club ya jijini Kinshansa.
AS Vita Club ndio wapinzani wakubwa wa Mazembe katika soka la DR Congo ambapo kibaya zaidi mastaa wote hao hakuna hata mmoja ambaye amewahi kuvaa uzi wa kuitumikia TP Mazembe na leo wanakutana tena wakiwa na Yanga.
Katika mazoezi ya Yanga mastaa hao ndio wameonekana kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wenzao wakitaka ushindi dhidi ya wapinzani wao hao ambao wako nao katika kundi moja la D kwenye mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati Bangala akiliamsha hivyo, Mayele naye ameliamsha kivyake akisema anajua hajafunga katika mechi kama nne zilizopita za timu yake lakini mashabiki wao waje uwanjani kutetema.
Mayele ambaye ni staa wa ufungaji mwenye jina kubwa kuliko staa yeyote wa Yanga alisema kambini kwao kuna mzuka ni mkubwa na kwamba wanahitaji matokeo katika mechi yao hiyo ya pili ya makundi baada ya kupoteza dhidi ya US Monastir ya Tunisia.
“Najua kuna mechi zimepita bila kufunga lakini niwaambie wananchi waje uwanjani kesho (leo) waje tuteteme pamoja, tunahitaji ushindi katika mchezo huu muhimu,” alisema Mayele. Yanga ina kumbukumbu ya kufungwa na Mazembe nje ndani mechi za makundi ya Shirikisho mwaka 2016 kwa mabao 1-0 na 3-0.