Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bangala alivyowang'oa Muguna, Ndala Azam!

Yannick Bangala 3333 Yannick Bangala amejiunga na Azam FC

Tue, 1 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

"BANGALA karibu Mbagala," ndivyo lilivyosomeka chapisho la Azam FC kwenye ukurasa wake wa Instagram lilitangaza ujio wa kiraka Yannick Bangala kutoka Yanga SC.

Bangala amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam baada ya kudumu Yanga kwa miaka miwili pia. Alijiunga na miamba hiyo ya Jangwani msimu wa 2021/22 akitokea FAR Rabat ya Morocco ambayo pia alijiunga nayo mwaka 2020 akitokea AS Vita ya Kinshasa DRC.

Bangala ambaye ni MVP wa Tanzania wa msimu wa 2021/22, hakupata nafasi sana msimu wa 2022/23 ambao ulikuwa bora sana kwa Yanga.

KUJIUNGA AZAM FC

Bangala ni chaguo la Kocha, Yousouph Dabo katika eneo la kiungo cha ulinzi ambalo anaamini hana mtu sahihi zaidi ya Sospeter Bajana pekee.

Itakumbukwa kwamba katika eneo hilo Azam FC ilikuwa na watu watatu msimu uliopita; Bajana, Issa Ndala na Kenneth Muguna.

Ndala, raia wa Nigeria, alijiunga na Azam msimu wa 2022/23 akisaini mkataba wa mwaka miwili. Muguna, raia wa Kenya, alijiunga na Azam msimu wa 2021/22, akisaini mkataba wa miaka miwili. Kenneth Muguna mkataba wake ulikuwa inaisha mwishoni mwa msimu uliopita na Azam ikamuongezea mwaka mmoja.

Kocha Yousouph Dabo ambaye Azam ilishafanya naye mawasiliano na makubaliano, alisema hawaoni hao kama wachezaji sahihi kwa klabu hiyo.

Kuna wakati alikuja na kukaa hapa kwa takribani miezi miwili akiifuatilia timu kiufundi na tabia za wachezaji. Alimsoma mchezaji mmoja mmoja na katika ripoti yake akashauri moja kwa moja Muguna aachwe japo alishasaini mkataba mpya.

Kisha akasema Issa Ndala ambaye alibaki na mwaka mmoja, asiongezewe mkataba. Katika eneo la kiungo cha ulinzi, ni Sospeter Bajana pekee ndio aliyeshauri aongezewe mkataba halafu akaomba kumuona kwa karibu Samuel Jackson Onditi ambaye alikuwa kwa mkopo Ihefu.

Akataka aungane na timu kwenye kambi ndogo ya maandalizi kabla ya msimu iliyofanyika Chamazi kabla ya safari ya Tunisia.

Akaondoka na kurudi kwao Senegal akisubiri kambi ya maandalizi itakapoanza aje tena Tanzania na ndivyo ilivyokuwa.

Ndipo 'Thank You' ilivyomhusu Muguna, yaani aliondoka Azam akiwa ameshasaini mkatana mpya. Kazi ikabaki kwa Ndala. Wakurugenzi wa Azam walikuwa wakimkubali sana huku wachambuzi wengi nchini wakimwagia sifa.

Kutokana na sifa za wachambuzi, wakurugenzi wakahisi kwamba wataonekana hawako 'serious' mbele ya jamii endapo watamuacha mchezaji wao bora...wakampa mkataba mpya. Dabo aliporudi na kuanza kazi rasmi pale Chamazi, akaambiwa Onditi amekataa kuja, hivyo Ndala aliongezewa mkataba.

Akasikitika sana. Akaomba kikao na wakurugenzi kuelezea kwanini hakutaka wachezaji wale wawili waendelee kubaki ndani ya Azam.

Wakurugenzi wakamuelewa na kumpa kazi yeye mwenyewe kutafuta mtu sahihi anayemtaka. Akatoa orodha kadhaa ya wachezaji anaowataka ambao kimsingi wote walikuwa wakicheza nje ya Tanzania. Uongozi ukaanza harakati za kuwatafuta lakini haikuwa rahisi kupatikana. Ndipo ikaibuka habari ya Bangala kwamba hana mahusiano mazuri na Yanga.

Yousouph Dabo anamfahamu Bangala kwa sababu wakala wa Bangala pia anasimamia wachezaji kadhaa ambao Dabo ameshafanya nao kazi na kupitia mstari huo ndipo akamfahamu Bangala. Akaushauri uongozi ufanye mawasiliano na Yanga kwa sababu alipata taarifa kwamba hawana mipango naye.

Lakini uongozi wa Azam haukutaka hata kidogo kurudi Yanga baada ya sakata la Feisal Salum 'Fei Toto'. Bangala aliongea na Dabo tangu kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) uliopigwa jijini Tanga na kumuelezea hali yake ndani ya Yanga. Kwa hiyo kocha akaendelea kuwapiga presha wakurugenzi kuhusu Bangala.

Lakini Wakurugenzi hawakutaka kuchukua hatua yoyote kwa hofu mbili; kwanza kuonekana wao ndiyo chanzo cha mgogoro wa Yanga na Bangala na pili kuvunja mkataba na Ndala ambaye alisaini mwishoni mwa msimu uliopita.

Dabo akaendelea kusisitiza kwamba hamtaki Ndala kwenye kikosi chake na hawezi kucheza na kiungo mmoja tu wa ulinzi msimu mzima.

Kwa kadiri wakurugenzi walivyozidi kuchelewa, ndivyo Dabo alivyowapiga presha na kusema 'sababu kubwa ya kukwama Azam ni mambo kama hayo'.

Akiwa Tunisia, inaelezwa Dabo aliomba kikao cha mtandaoni na viongozi hao na kuwasisitiza umuhimu wa kupata mtu sahihi katika eneo la kiungo cha ulinzi na kumtoa Ndala.

Wakurugenzi hao ambao wamemuelewa sana kocha huyo kutokana na uchambuzi wake alioufanya alipokuja mara ya kwanza na kutoa taarifa yenye majibu kwa maswali yao...wakasalimu amri na kufanya anavyotaka.Wakafanya mawasiliano rasmi na Yanga kuhusu Bangala.

Yanga ambao nao walikuwa na kesi na Bangala, wakaona afadhali wautue mzigo, wakakaa mezani na kutaka dau la Dola 50,000 za Marekani (zaidi ya Sh120 milioni za Kitanzania). Taratibu zikafuatwa...Bangala akaenda Mbagala na Ndala akarudi Nigeria.

Chanzo: Mwanaspoti