BEKI wa kati wa Klabu ya Mtibwa Sugar ya Manungu Turiani Abdi Banda ameingia katika sekeseke zito kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoa kauli chonganishi juu ya hujuma na mbinu chafu inayotumia Klabu ya Simba katika michezo yake ya kimataifa.
Kwa mujibu wa gazeti la KickOff la nchini Afrika kusini limedai kuwa Klabu ya Simba inatumia mbinu chafu katika kushinda michezo yake ya kimataifa ikiwemo kuwahonga waamuzi lakini pia kupata msaada kutoka kwa wanasiasa waliopo ndani ya Serikali ya Tanzania.
Gazeti hilo limemnukuu Abdi Banda kama sehemu ya chanzo cha habari kutokana na kuwa na historia ya kucheza katika klabu ya Simba lakini pia kucheza kwenye ligi ya Afrika Kusini kwenye klabu ya Baroka Swallows na Highlands Park.
Gazeti hilo limeainisha kuwa Banda anaamini Orlando Pirates watafuzu kutokana na sababu kwamba mchezo wao wa kwanza utaanzia Dar es Salaam ambako wanatakiwa kuwa makini wasiruhusu kufungwa ili iwe rahisi kwao kwenda kumalizia mchezo Johannesburg.
“Pirates lazima wamtumie Senzo kwenye safari yao ya Tanzania kwa sababu anaijua vizuri Tanzania na ameshawahi kufanya kazi na Simba na sasa yupo na Yanga.
“Yanga watakuwa tayari kuwasaidia Orlando katika namna yoyote ile watakayotaka kwa sababu Yanga na Simba ni maadui.” Amesema Abdi Banda.
Klabu ya Simba Aprili 17 itawakaribisha Orlando Pirates katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.