Beki wa Richardsbay FC, inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Mtanzania Abdi Banda amesema haoni ubaya kusajiliwa wachezaji wengi wa kigeni, ila anaona itofautishe na mipango ya timu ya taifa.
"Wachezaji wa kigeni wanakuja kutupa changamoto wazawa, lakini idadi ya wachezaji 12 kucheza wote hapo ndipo ninapowaza kwa maslahi mapana ya Stars, kwani hao 12 wanapocheza je mzawa anapata wapi muda wa kucheza.
"Kwa nchi kama Morocco inalimiti ya kusajili wageni, hivyo hata sisi tungefikilia zaidi kuhusu Stars, nasema hivyo mimi ni mchezaji wa Stars, lazima niumie kuhusiana na hilo,naangalia ndani ya vilabu vinavyosajili wachezaji wazawa wengi wanapoteza nafasi ya kucheza sasa wakiitwa timu ya taifa watafanya nini.
"Mfano Yanga wamesajili mabeki wengine wageni ina maana Dickson Job atakaa benchi ama anaweza akawa chaguo la nne, akiitwa Stars wakati hachezi itaisaidiaje Stars?, nadhani inatakiwa kuandaliwa vitu vilivyopo kwenye mifumo vya kuleta maendeleo ya taifa." amesema Banda akichangia mjadala unaoendeshwa kwenye mtandao wa X na kampuni ya Mwananchi Communications Limited.