Kikosi cha AS Real Bamako kimekubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga huku kiungo wake mahiri, Ibrahim Sidibe akitaja sababu iliyowapoteza ni kiwango cha mshambuliaji, Fiston Mayele.
Bamako ilikubali kichapo hicho katika mchezo wa kundi ‘D’ Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mechi ya kwanza iliyopigwa Mali kufungana 1-1.
Akizungumza Sidibe alisema kitendo cha wao kuruhusu bao la mapema la Mayele dakika ya nane ya mchezo kilichangia kuwatoa mchezoni licha ya kucheza vizuri.
“Lengo letu lilikuwa ni kulinda kwanza huku tukishambulia kwa tahadhari kwani tuliamini hii ni silaha kubwa kwetu kwa sababu tunacheza ugenini ingawa jitihada zake binafsi zilifanikiwa.”
“Kiujumla tulicheza vizuri isipokuwa makosa binafsi na matumizi mazuri ya nafasi kwa wapinzani wetu yaliweza kutugharimu hivyo kutuweka kwenye mazingira mabaya ya kufuzu hatua inayofuata.
” Kichapo hicho kimeifanya Bamako kubaki mkiani na pointi zake mbili huku Yanga ikiwa ya pili na pointi saba wakati US Monastir ikiwa timu ya kwanza kufuzu kundi hilo baada ya kufikisha pointi 10.
TP Mazembe ambayo ilichapwa juzi na Monastir kwa bao 1-0 inashika nafasi ya tatu.