Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balozi Bwana awapokea Wananchi Sauzi

Balozi Ta Balozi Bwana awapokea Wananchi Sauzi

Tue, 2 Apr 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, ameongoza mapokezi ya kikosi cha timu ya Young Africans SC ilipotua Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Kikosi hicho kilitua Afrika Kusini mchana wa leo kwa Ndege ya Shirika la Malawi baada ya kuondoka Dar es Salaam alfajiri kikiwa na wachezaji 26 na viongozi 12 wa benchi la Ufundi.

Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo uliopo Johannesburg, Afrika Kusini, mashabiki na wanachama wa Young Africans waliopo nchini humo waliupokea msafara huo, kisha Balozi James Bwana akapata wasaa wa kutoa neno.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa niaba ya Ubalozi wa Tanzania hapa Afrika Kusini, tumejiandaa vema, basi tuwatakie kila la kheri katika matayarisho katika kuelekea katika mchezo wetu,” alisema kiongozi huyo.

Naye Rais wa Klabu ya Young Africans, Eng. Hersi Said, alisema: “Tunawashukuru wanachama na wapenzi wa Young Africans na wale sio wa Young Africans ambao wameacha shughuli zao hapa South Africa na kuja kujumuika na sisi.

“Zaidi ya hapo Mheshimiwa kikosi kipo tayari, kocha na benchi la ufundi wote wako vizuri na tunataraji Inshaallah siku ya Ijumaa tunakwenda kupigania bendera ya taifa letu kwa sababu sio tu nembo ya Yanga inakwenda kupandishwa hapa, lakini pia ni Taifa letu la Tanzania.”

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Lameck Nyambaya, ambaye ameambatana na timu, amesema: “Sisi kama viongozi tumekuja kwa ajili ya kuipigania nchi yetu, tumekuja kuipigania Yanga, niwahakikishie kwamba tutaondoka na ushindi.”

Ikumbukwe kwamba, Young Africans SC ipo Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaochezwa Ijumaa ya Aprili 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld uliopo Pretoria nchini humo baada ya ule wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam, kumalizika kwa matokeo ya 0-0.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live