Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baleke na Phiri? Hebu msikie Jobe

Pa Omar Jobe Simba SC Baleke na Phiri? Hebu msikie Jobe

Mon, 5 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati mashabiki wa Simba wakiwa bado wanajiuliza namna timu yao itakavyoweza kuyarudisha mabao ya Jean Baleke na Jenerali Moses Phiri, straika mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Pa Omary Jobe ametoa neno muhimu akisema "mtasahau shida zote."

Simba haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo ambao ulienda kwa Yanga huku pia wakikumbana na kipigo cha kudhalilishwa cha mabao 5-1 kutoka kwa mahasimu wao hao wa Jangwani.

Ili kurejesha utawala wa misimu minne ambayo Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mfululizo kabla ya utawala kutua kwa Yanga misimu miwili iliyopita, Wekundu wa Msimbazi waliamua kwanza kuachana na kocha Mbrazili Roberto Oliveira 'Robertinho' na kumleta Abdelhak Benchika na kuachana na mastraika Baleke na Phiri na kujaza nafasi zao kwa kuwashusha Pa Jobe na Freddy Michael.

Sasa, Pa Jobe ambaye alianza kwa kutupia bao katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), ambayo Simba ilishinda 4-0, ametoa kauli za kishujaa akisema akizoea mbona atafunga sana tu.

Nyota huyo kutoka Gambia, ambaye aliingia 'sub' wakati Simba ilipoifunga Mashujaa 1-0 katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara Jumamosi, ameliambia Mwanaspoti amefurahi kuwepo kwenye timu hiyo na kukiri anajua mtihani unaomkabili, lakini aliwatuliza mashabiki akisema kufunga mabao ndio kazi yake ila akawaomba wampe muda kwanza.

“Simba ina viungo wazuri na mabeki wazuri wa pembeni wenye ubunifu na kama nitazoeana nao kwa haraka basi najipanga kuwa na mwendo mzuri wa kufunga. Nina shauku kubwa ya kujua pia ubora wa ligi kwa maana ya timu pinzani na ushindani ulivyo ili nijue jinsi ya kujipanga kwenye mechi hizo,” amesema Pa Jobe anayefahamika pia kwa jina la utani la Drogba akifananishwa na nyota wa kimataifa wa zamani wa Ivory Coast, Didier Drogba aliyewahi kuwika na klabu mbalimbali barani Ulaya ikiwamo Chelsea.

Pa Jobe aliyeacha rekodi Senegal ya kuwa Mfungaji Bora kipindi akicheza pamoja na kiungo wa sasa wa Simba, Babacar Sarr kabla ya kwenda Ulaya, ana kazi ya kujihakikishia namba mbele ya nyota wengine wa timu hiyo akiwamo Freddy na Kibu Denis na mkongwe John Bocco katika eneo hilo la ushambuliaji.

Mapema, kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amewazungumzia wachezaji hao wapya kwa kusema hana hofu nao kwani wote wanaonekana wana uwezo, ila ni ngumu kuanza kuwapima kupitia mechi moja au mbili, akiamini kadri watakavyopewa nafasi kikosini watazidi kuimarika na kuwapa furaha wanasimba.

Kikosi hicho cha Simba kinajiandaa kuvaana na Tabora United katika mechi nyingine ya kiporo itakayochezwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kabla ya kuhamia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuikaribisha Azam katika mechi ya kiporo cha Mzizima Derby itakayopigwa Februari 9.

Mechi hiyo ya Mzizima Derby imepelekwa Kirumba, baada Simba kuuchagua kama uwanja wa nyumbani kutokana na Uhuru kufungwa na serikali sambamba na ule wa Benjamin Mkapa ili kupisha ukarabati.

Tarehe hiyo ilipangwa baada ya kuahirishwa mara mbili kutoka muingiliano michuano ya Afcon 2023 na michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Mchezaji huyo amesema anafurahi kwa kocha kumuamini na kumpa nafasi katika michezo yote miwili tangu ajiunge na timu hiyo, lakini amesema wamsubiri kidogo kwa sababu ndio kwanza anacheza soka nchini.

Amekiri ni kweli Simba ina mastaa wengi wenye ubora wa hali ya juu wenye uwezo wa kutoa matokeo muda wowote, kitu ambacho kwake ni faida kwa nafasi anayocheza na kadri atakavyozoeana na wenzake ndivyo atakavyokuwa mtamu, hivyo mashabiki wawe na subira.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: