Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baleke amuondoa staa Simba

Baleke Awapiga Ihefu.jpeg Jean Baleke

Wed, 12 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ubora wa mshambuliaji wa Simba, Jean Baleke umemuondoa kwenye kikosi cha kwanza, Moses Phiri huku kocha Mbrazil Roberto Oliviera ‘Robertinho’ akikiri kwamba itamlazimu kuwa mvumilivu sana sambamba na kufanya kazi ya ziada mazoezini.

Baleke tangu amesajiliwa na Simba ameifungia timu hiyo mabao 12 kwenye mashindano yote, ambayo kwenye ligi ametupia matano, ASFC manne na Ligi ya Mabingwa Afrika amefunga mabao matatu, Phiri kafunga mabao 10 kwenye ligi na FA kafunga mabao manne jumla yakiwa 14 lakini akiwa ameanza nayo kuanzia mwanzo wa msimu.

Akizungumza Robertinho alisema Phiri ni mchezaji mzuri na amekuwa mmoja ya wachezaji walioipambania timu lakini kwa sasa ni ngumu kurudi kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja kutokana na mchezaji ambaye amepata nafasi ya kucheza chini yake kufanya kazi kwa ubora.

“Nafahamu Phiri ndiye kinara wa upachikaji mabao, nimemkuta na kikosi akiwa ametoka majeruhi hivyo nafasi yake imechukuliwa na Baleke ambaye pia anafanya kazi yake kwa usahihi ananipa kile ninachokitaka, sina jinsi.

“Hivyo kumrudisha Phiri kikosini inahitaji muda zaidi kwani hayupo fiti na ili aweze kurudi anatakiwa kucheza mara kwa mara na nafasi hiyo siioni kwasababu timu inahitaji matokeo zaidi na sio kumrudisha mchezaji kwenye ubora,” alisema.

Robertinho alisema atakuwa anampa muda wa kucheza dakika chache ili kurudisha kwenye ubora wake anamuamini na anatamani kuona anarudi ili kusaidiana na Baleke na kuendelea kuifanya Simba iwe bora kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Alisema uwepo wa Baleke ambaye amekuwa akifunga kwenye kila mchezo anaopata nafasi ya kucheza unamfanya amuongezee mbinu ya kumuweka fiti zaidi ili aweze kumpa kile anachostahili huku akikiri kuwa ni moja ya wachezaji wapambanaji na wasikivu kwenye uwanja wa mazoezi na ndio maana anakuwa bora.

“Kila mchezaji ana mchango wake kwenye kikosi hata huyo Baleke asingeweza kufunga bila ushirikiano mzuri na wenzake hivyo naamini Phiri akiwa kwenye hali nzuri atarudi kwenye nafasi na ataongeza ushindani lakini lazima apambane sana;

“Timu ikiwa na wachezaji wenye uwezo sawa inaongeza ushindani kwenye nafasi yoyote kwenye uwanja wa mazoezi na kunipa changamoto kuamua nani aanze na nani aanzie benchi.”

Chanzo: Mwanaspoti