Kocha Mbrazil wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' ameendelea kukikonoa kikosi hicho huku akiwataja wachezaji wapya akiwamo Ismael Sawadogo na Jean Baleke wakimzpa mzuka kama ilivyo kwa nyota waliokuwa majeruhi akiwamo Moses Phiri na Peter Banda.
Akitoka kuiongoza Simba kushinda mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City ikiwa ni mechi ya kwanza kwake kama kocha mkuu wa timu hiyo, Mbrazili huyo ametamba anaelekeza nguvu kubwa kwa mchezo ujao wa ugenini watakapoumana na Dodoma Jiji akisisitiza anataka mabao mengi na soka safi uwanjani.
Robertinho alisema bado hajapata kikosi chake cha kwanza lakini anaona mwanga kutokana na wachezaji wengi waliokuwa majeruhi kupona na wale waliosajiliwa dirisha dogo kuungana pamoja na kuamini wataisaidia timu kuimarika zaidi.
Phiri na Banda waliokuwa majeruhi sambamba na Ismael Sawadogo, Jean Baleke na Mohamed Mussa waliosajiliwa kwenye dilisha dogo lililofungwa Januari tayari wameanza mazoezi na timu jambo lililomfanya Robertinho kutamba.
"Siwezi kusema tayari nina kikosi cha kwanza, hapana. Nmekuta wachezaji wengine wanaumwa mfano Phiri na tumesajiliwa wapya kina Baleke, hivyo nahitaji kukaa nao wote wakiwa fiti ndipo nitapata kikosi cha kwanza," alisema Robertinho aliyetua Simba akitokea Vipers ya Uganda.
Hata hivyo hilo halijamzuia kocha huyo kuzungumzia ubora wa kikosi chake huku akisisitiza kila mchezaji kujituma zaidi kwani anaamini kila mmoja anaweza kupata namba kikosi cha kwanza na kuifanya Simba kuwa tishio zaidi kwenye michuano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
"Mwanzo nilikuambia nina vitu viwili akilini mwangu ambavyo nataka kuviingiza hapa Simba, moja ni timu kushinda kila mechi na mbili ni kucheza vizuri kwa kasi.
Kwa maana hiyo kila mchezaji anaweza kuwa bora kama atavitambua hivyo na kuvifanyia kazi," alisema kocha huyo na kuongeza;
Nadhani mechi na Dodoma inaweza kuwa tofauti na iliyopita, kuna wachezaji wapya wameingia kikosini na wengine waliokuwa majeraha wamerudi kama wataonyesha kitu kizuri mazoezini naweza kuwatumia. Pia wapo ambao waeanza kufanya vizuri, wanahitaji kuendelea kufanya hivyo kwa manufaa ya timu kwani lengo letu wote ni moja, kufikia malengo."
Simba inawania ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa nafasi ya pili ikikusanya pointi 47 baada ya mechi 20, nyuma ya vinara, Yanga yenye alama 53 na kesho itakuwa wageni wa Dodoma yenye pointi 20 katika nafasi ya pili katuika mechi itakayopigwa Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.