KAIMU Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Juma Mwambusi amesema anafurahia kurejea kwa kiungo wake Mapinduzi Balama ambaye amevua soksi ngumu (POP) na yuko mbioni kurejea uwanjani.
Kiungo huyo aliumia mazoezini alipokuwa akijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC ‘Wanakuchele’ mwaka 2019 na tangu hapo hajaonekana uwanjani.
Mechi ya mwisho kumshuhudia Balama uwanjani akiwa na jezi ya Yanga ilikuwa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Namungo ambao uliisha kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza na gazeti hili, Mwambusi alisema kuwa ni taarifa njema kwake kurudi kwa kiungo huyo ambaye anakuja kuongeza nguvu katika safu yake ya kiungo na kuongeza wigo wa wachezaji katika kikosi chake.
“Hizi ni taarifa njema kwa benchi la ufundi la Yanga, pamoja na mashabiki wa timu yetu ambao walikuwa na hamu ya kumuona Balama akirudi na kuendeleza mapambano,” alisema Mwambusi.
Mwambusi alisema kuwa hivi sasa akili yake ipo katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC mtanange ambao utapigwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa Aprili 7 mwaka huu.