Changamoto katika maisha ni vitu vya kawaida, lakini kuna nyingine huwa zinakatisha tamaa na kama mtu ana roho ndogo ni ngumu kutoboa.
Hutokea bahati tu, mtu akizungukwa na watu wenye kujali na kutia moyo na kusaidia ushauri wa kisaikolojia kama ilivyomkuta winga wa zamani wa Yanga, Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’ anayefichua alivyobakia kidogo tu aache kucheza soka kutokana na jeraha la mguu lililochanganya akili.
Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, nyota huyo anayekipiga kwa sasa Mashujaa Kigoma baada ya kupitia Mtibwa Sugar na Coastal Union, mara alipoachana na Yanga amefunguka mambo mengi na jinsi majeraha yalivyotaka kukatiza ndoto zake za soka na kama isingekuwa viongozi wa Wanajangwani, angekuwa ameondoka kwenye ramani ya karia yake.
MSIKIE MWENYEWE
“Kuna wachezaji wengi wanatoka mchezoni kutokana na kukosa watu sahihi wa kuwashika mkono, inapotokea wanapita kwenye changamoto ngumu, nilijifunza hilo kwenye mapito yangu ya kukaa nje ya kazi miaka miwili na nusu,” anasema.
Anasema ni rahisi mchezaji kupotea kwenye ramani ya soka, endapo akikumbana na changamoto za majeraha ya kumweka nje kwa muda mrefu, anakuwa anakosa jinsi ya kujikimu kimaisha.
CHANZO HIKI HAPA
Balama alisajiliwa na Yanga, Juni 22, 2019 akitokea Alliance ya Mwanza, mkataba uliokuwa wa miaka mitatu, msimu wa kwanza ambao pia hakuumalizia ndio uliompa furaha uwanjani.
Anasema baada ya kuumia katikati ya msimu wake wa kwanza, akiwa mazoezini alifungwa hogo, alilokaa nalo miezi mitatu, hivyo akawa na matarajio akilifungua atakuwa amepona kabisa.
“Baada ya miezi mitatu, Yanga ilituma vipimo vyangu Afrika Kusini, wakaambiwa hali ya mguu wangu ni mbaya, inatakiwa nikae mwaka bila kufunga kitu chochote, baada ya hapo ndio niende wakanifanyie upasuaji, kauli hiyo iliniumiza na kunivunja moyo, nikatamani kuachana na soka kabisa,” anasema Balama na kuongeza;
“Viongozi wa Yanga walijitahidi kunijenga ili nisitoke kwenye mstari, muda ulipofika wakanipeleka Afrika Kusini, nikafanyiwa upasuaji, hivyo isingekuwa rahisi kurejea kwenye kiwango kwa haraka.
“Wakati najiunga Yanga ilikuwa kati ya ndoto zangu kucheza timu mojawapo kongwe hapa nchini, hivyo hamu ya kuonyesha kipaji changu ilikuwa kubwa, bahati mbaya sikutimiza kile nilichokitarajia, hicho ndio kitu kilichoniumiza na sitakisahau kwenye maisha yangu.”
MSONGO WA MAWAZO
Anasema baada ya kuondoka Yanga kwenda Mtibwa Sugar, alikuwa na msongo wa mawazo, alisaidiwa na Kocha Salum Mayanga alimjenga na kumwamini kumpa miezi sita ya mkataba.
“Wakati naondoka Yanga akili ya kazi ilikuwa haipo kabisa, Kocha Mayanga aliliona hilo na siyo rahisi kocha kukuchukua wakati ulikuwa huchezi, akasema nitulize akili, akawa ananipa mechi mara kwa mara, wachezaji wakawa wananipa moyo, kisha nikajikuta naanza kurejea taratibu mchezoni,” anasema Balama na kuongeza;
“Wachezaji wa Yanga ambao muda wote walikuwa wananipigia simu na wanapiga hadi sasa ni Kibwana Shomari, Dickson Job na Aboutwalib Mshery, wamenisaidia pakubwa kuhakikisha nakaa sawa, wananiambia jitume bado una umri mdogo, kiwango chako kikubwa, una uwezo wa kucheza klabu yoyote hapa nchini.”
Anasema baada ya kujiunga na Mashujaa, anaona ameanza kurejea kwenye kiwango chake, anajibidiisha kuhakikisha, anafanya makubwa ya kutimiza ndoto zake ikiwezekana kucheza soka nje.
“Kutokana na matukio ya wachezaji kuumia, tunaomba suala la Bima ya Afya litiliwe mkazo, najiuliza nilivyoumia nisingekuwa Yanga huenda ungekuwa mwisho wangu wa kucheza soka, kwani changamoto kama hizo zinaweza zikamkuta mchezaji yoyote nje ya klabu zenye uwezo wa kutibu wachezaji nje.”
JINA LA KIPENSELI
Anasema mikato ya masela wa Iringa, salamu zao za kijiweni wakisalimiana, mfano mtu akimwambia mwenzake mambo vipi, anayejibu ni kama kipenseli, akimaanisha mambo yake yamenyooka.
Baada ya washkaji zake kujua ni mzaliwa wa Iringa, wakampachika jina hilo, hata hivyo anasema halipendi, ajabu anaona ndio kwanza linamganda.
“Nyumbani Iringa ni salamu ya wahuni, nikisema wahuni sina maana wanakaba watu, ila wale ambao hawana muda wa kujua nani anafanya nini, kifupi wapo bize na maisha yao, hivyo wakiitikia salamu ya mambo wanajibu kama kipenseli, wakimaanisha yamenyooka,” anasema Balama na kuongeza;
“Kiukweli hilo jina silipendi kabisa, ila sijui kwa nini washikaji zangu wananing’ang’ania kuniita, kuna wakati siitiki kabisa, maana naliona halina maana yoyote.”
MKULIMA IRINGA
Balama aliyewahi kusoma kozi ya jeshi, anasema nje na soka analima mazao ya biashara mkoani kwao Iringa, hivyo akija kutundika daluga ataendelea na shughuli zake hizo.
“Nikimaliza soka, sitahitaji mambo ya kusomea ukocha, sisi tunaokaa na makocha tunaziona presha zao, mwezi mmoja yupo kwenye timu, unaofuata unafukuzwa, timu ikifanya vizuri wanashangiliwa, ukifanya vibaya kibao kinageuka, maisha kama hayo mimi siyawezi kabisa,” anasema Balama na kuongeza;
“Kulima mazao ya biashara nilianza muda mrefu, ingawa kukaa kwangu Yanga kumenirahisishia kumiliki vitu kirahisi zaidi, tofauti na nilivyokuwa nategemea mazao pekee.”
Mbali na hilo, anasema umarufu kuna wakati mwingine unaumiza, akitolea mfano namna mashabiki walivyokuwa wanasema ndio mwisho wake wa soka, baada ya kutemwa Yanga Julai 14, 2022.
“Japo sikuwahi kusemwa vibaya na mashabiki wa Yanga, kulikuwa na wale ambao walikuwa wanaandika maskini kijana wa watu, soka ndio basi tena, maneno hayo yalikuwa yananikata sana, kwani nilikuwa nimekata tamaa sana, nilitamani kupata mtu wa kuniambia songa mbele, ndio maana sitakaa nimsahau kocha Mayanga kwenye maisha yangu,” anasema Balama anayependa aina ya uchezaji wa Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Nje na hilo, anaizungumzia Simba licha ya kufungwa na Mashujaa kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA), anaona ina kikosi kizuri, isipokuwa wachezaji, wajitoe kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Mfano tulivyowatoa kwenye michuano ya FA, tulichowazidi, sisi tulijitoa zaidi, kitu kinachowezekana hata wao kukifanya na mashabiki wao, wataona kumbe walikuwa na bonge la timu,” anasema winga huyo mwenye mbio uwanjani.
CHARLES NDUKI
Mwanasaikolojia Charles Nduki anasema kuna haja klabu za soka ziwe na watu wa saikolojia, kwani makocha na wachezaji wanakuwa wanapitia changamoto zinazokuwa zinahitaji msaada wa kiakili.
“Japo makocha wengi wamesomea saikolojia, lakini wanakuwa na mzigo mzito, pindi timu zao zinapokuwa zinakosa matokeo, aumize akili kuhusu mbinu pia aanze kudili na mchezaji mmoja mmoja kwenye matatizo ya kiufundi na nje ya kazi,” anasema.