Wachezaji wawili ambao walikuwa nje ya uwanja kwa muda tofauti katika kikosi cha timu ya Wananchi Yanga wamerejea kukipiga kunako klabu hiyo baada ya kupata nafuu na kupona kabisa.
Wachezaji hao ni viungo Dickson Ambundo na Balama Mapinduzi wamepona majeraha yao na sasa wanaweza kuanza kukichafua rasmi kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi.
Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema; “Tuna wachezaji wengi bora na tutawatumia katika mechi zijazo, Ambundo na Balama wamerejea kutoka kwenye majeraha hivyo watakuwepo kwenye Kombe la Mapinduzi na michezo mingine ijayo kwani viwango vyao ni vizuri.
“Ukiwa na kikosi cha wachezaji wengi bora unatakiwa utafute namna ya kuwapa nafasi ya kucheza,” alisema.
Ambundo ni ingizo jipya kutoka Dodoma Jiji lakini tangia usajili wake amekuwa akiingia na kutoka kwenye kikosi kutokana na majeruhi.