Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balaa zito! Pep ajitabiria kifo mapema

Pep Guardiola Qatar Meneja wa Man City, Pep Guardiola

Fri, 13 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati ikiwa imebakia siku moja kabla ya mabingwa watetezi, Manchester City kuumana na mahasimu wao Manchester United kwenye ile Manchester Derby, kocha wa Man City, Pep Guardiola ametupa taulo mapema na kusisitiza kwamba haoni nafasi ya wao kupata ushindi.

Mechi hiyo ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Old Trafford ni muhimu kwa timu zote mbili katika harakati za kuelekea ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu.

Katika siku za hivi karibuni Man City imekuwa na rekodi nzuri mbele ya Man United kwenye EPL ambapo kwenye mechi nne Man United imefungwa tatu mfululizo kuanzia mwaka juzi na mara ya mwisho United kushinda mechi ya ligi ilikuwa Machi, 2021.

Lakini kiwango cha Man City katika mechi za ligi kwa siku za hivi karibuni kimekuwa na panda shuka nyingi ambazo kwenye mechi nne za mwisho, imeshinda mbili, imefungwa moja na sare moja.

Vilevile imetupwa nje ya michuano ya Carabao juzi, baada ya kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Southampton kwenye hatua ya robo fainali.

Katika mechi hiyo Man City iliweka rekodi mbaya ya kutopiga shuti lolote langoni ikiwa ni mara yao ya kwanza kwenye michuano yote tangu Aprili 2018 ilipokutana na Liverpool.

Pep anaeleza kuwa wachezaji wake wengi wamepoteza umakini wawapo uwanjani hali inayosababisha wasicheze vile inavyotakiwa na mwisho hujikuta wakiruhusu mabao na kupoteza mechi.

“Unatakiwa ujiandae kiakili kama mchezaji kwenye kila mechi unapokuwa unaichezea Manchester City, kama tutacheza kwa staili hii kwenye mchezo wetu dhidi ya Man United, hatuwezi kushinda hata kidogo, sidhani kama nilikosea kuanza na wachezaji nilioanza nao, tumefungwa mechi ya leo (juzi dhidi ya Southampton) kwa sababu hata akili zetu hazikuwa uwanjani.”

Kitendo cha kuitoa Man City kwenye michuano hiyo, kilimpa nafasi ya kupumua kocha wa Southampton, Nathan Jones kwani inakuwa ni mechi ya pili ya kushinda baada ya kuwa kwenye mwenendo mbaya ikiwa inashikilia mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Man United italazimika kushinda mechi hii ili kupanda hadi nafasi ya tatu na kuishusha Newcastle kwa kufikisha alama 38, wakati Man City pia ikishinda itakuwa imepunguza tofauti ya alama tatu dhidi ya wapinzani wao Arsenal waliopo kileleni mwa msimamo wa ligi.

Hii sio mara ya kwanza kwa Pep kuonyesha kwamba msimu huu hana chake kwani siku kadhaa zilizopita pia aliwahi kufunguka kwamba hadi sasa ni Arsenal na Man United ndio zina nafasi kubwa za kutwaa ubingwa kutokana na viwango wanavyoonyesha kwenye michezo yao ya hivi karibuni.

“Faida ambayo Arsenal na Manchester United wanazo kwa sasa ni kwamba msimamo uko wazi, ukicheza nao unaona kabisa kuna ile harufu ya kuandika historia, nafikiri hii inaweza kuwa nafasi nzuri kwa Arsena kuandika historia ya kuchukua taji hili kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu kwenye historia yao.

“Kama Arsenal itaendelea na moto huu huu, itakuwa ngumu sana kwetu kuweza kuwafikia na kuwavuka. Wanaweza kufikisha hata pointi 100 kwa mwendo huu.”

Chanzo: Mwanaspoti