Simba Sc imesajili kipa Mbrazil, Jefferson Luis kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Resende ya nchini kwao akitarajiwa kuwa mrithi wa Beno Kakolanya aliyetimkia Singida FG, sambamba na kuziba pengo la Aishi Manula atakayekaa nje ya uwanja hadi Novemba mwaka huu baada ya kufanyiwa oparesheni ya nyonga.
Usajili wa Jefferson umezua maswali mengi kwa mashabiki na wadau wengi wa soka nchini kutokana na daraja alilotoka lakini haya ni mambo matano yatakayomfanya acheze Simba.
Mosi, Moja ya vitu ambavyo wadau wamehoji ni pamoja na uwezekano wa kipa huyo kupata kibali cha kucheza Bongo licha ya kutoka timu ya kawaida nchini kwao Brazil.
Katika kanuni ya ligi namba 62 inayohusu wachezaji wa kigeni inaeleza; "Mchezaji wa kigeni anayeruhusiwa kusajiliwa kwenye ligi kuu ni yule anayecheza katika timu ya taifa ya nchi yake au Ligi Kuu ya nchi husika. Mchezaji kutoka Ligi Amerika ya Kusini na Ulaya lazima awe amecheza angalau kuanzia Ligi Daraja la Tatu (Kitaifa kutegemeana na mfumo wa nchi husika)."
Kwa maana hiyo Jefferson atapata vibali vya kucheza nchini kutokana na Brazil kuwepo na mfumo wa ligi kuchezwa kwa majimbo na yeye kutokea Resende timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza ya jimbo la Rio de Janeiro, ambayo ni miongoni mwa ligi za madaraja matatu ya juu nchini humo.
Pili, Wadau wamekuwa wakihoji juu ya uwezo wake kwani wasifu wake unaonesha amecheza timu sita tofauti lakini tano kati ya hizo alikuwa akienda kwa mkopo kutokea Resende na sasa katua Simba wakihofia kutofanya vizuri.
Jefferson ametua Simba wakati ambao timu hiyo haina kipa namba moja wake Manula (mgonjwa) na namba mbili Beno aliyeondoka hivyo kukutana na kipa namba tatu (Ally Salim), na Bwanamdogo Hemed Feruz aliyepandishwa kutoka timu B, hivyo ana nafasi kubwa ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba mbele ya Ally na Feruz kwani ni pendekezo la kocha.
Tatu, Baadhi ya mashabiki wa Simba na wadau wamekuwa wakihofia Jefferson kushindwa kucheza Tanzania kutokana na mazingira ya soka letu na hali ya hewa sambamba na viwanja.
Bado Jefferson ana uwezo wa kuwaziba midomo mashabiki hao kwani baadhi ya viwanja vya Brazil havina tofauti sana na vya Bongo lakini pia hali ya hewa zinaendana.
Hata hivyo Bruno Gomes wa Singida United, Gerson Fraga aliyewahi kupita Simba na Andre Coutinho aliyepita Yanga waliweza kucheza vizuri katika hali hiyo hiyo ilihali walitokea Brazil.
Nne, Wadau wanahofia kuhusu lugha ya mawasiliano kwani Watu kutoka Amerika ya Kusini wamekuwa wakizungumza zaidi Lugha zao ikiwemo Kireno, lakini kwa soka la kisasa lugha imekuwa kama nyongeza tu kwani wajuzi wa mambo wanasema 'Lugha ya Mpira' ni moja.
Kuna wachezaji wengi hawajui wala kuelewa Lugha inayozungumzwa muda mwingi na makocha, timu zao lakini wanafanya vizuri uwanjani.
Tano ni ushindani dhidi ya makipa wengine wa Simba kwani ambapo baadhi ya wadau wanaamini Manula akipona atarejea kuchukua namba moja yake kikosini jambo ambalo linawezekana au lisiwezekane.
Kocha Mkuu wa Simba Oliveira Roberto 'Robertinho' katika moja ya mahojiano na gazeti hili alisema kikosini kwake atakayepata namba ni mchezaji anayejituma na kufanya vizuri.
"Wachezaji ni wengi na hawawezi kucheza wote, huwa natoa nafasi kwa wale wanaofanya vizuri zaidi mazoezini na pale wanapopata nafasi hivyo kila mchezaji katika eneo lake anatakiwa kupambana na kuhakikisha anakuwa bora zaidi," alisema Robertinho.