Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Balaa la Bocco lamkuna Mmachinga

Mwana Fa Bocco Balaa la Bocco lamkuna Mmachinga

Sun, 17 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bao moja lililofungwa na nahodha wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ kwenye ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Kagera Sugar juzi, limemfanya nyota huyo kuivuka rekodi ya mabao iliyokuwa inashikiliwa na mchezaji, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’.

Bocco ambaye huu ni msimu wa 16 kucheza Ligi Kuu Bara amefikisha jumla ya mabao 154 na kuipita rekodi iliyowekwa na Mmachinga aliyefunga 153 kuanzia 1993 hadi 2005 akiwa amezitumikia timu mbalimbali za Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga na Twiga Sports. Rekodi ya Mmachinga imedumu kwa miaka 18 bila kuvunja kabla ya juzi Bocco alipotokea benchi na kufunga bao la tatu dakika za majeruhi.

Rekodi zinaonyesha Bocco alianza kufunga mfululizo katika Ligi Kuu tangu alipoipandisha Azam daraja msimu wa 2008-2009 aliyodumu nayo kwa misimu tisa hadi 2016-2017 akiifungia jumla ya mabao 84 na alipohamia Simba 2017-2018 hadi msimu huu ukiwa ni wa saba ameifungia mabao 70.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya rekodi yake iliyodumu kwa muda mrefu kuvunjwa, Mmachinga alisema kwanza anashukuru aliyefanya hivyo ni mchezaji wa Tanzania huku akimmwagia sifa kutokana na uvumilivu alionao licha ya kukatishwa tamaa.

“Kwangu nampongeza kwa hatua aliyofikia kwa sababu ni mchezaji wa ndani ila hata ukiangalia amekuwa akisemwa kwa mengi ingawa hilo kwake hajawahi kuliweka akilini na badala yake anaendelea kuonyesha kipaji uwanjani kwa vitendo,” alisema Mmachinga.

Mkongwe huyo aliongeza kwa kusems anaamini Bocco ni mfano mzuri wa kuigwa na wachezaji wanaochipukia, kwani angekuwa anafuatilia mambo yanayosemwa asingeweza kufika hapa alipo hivyo ni moja ya washambuliaji ambao wanahitaji kuheshimiwa kwa mchango wao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live