Wakati Kiungo Mshambuliaji wa Young Africans, Stephane Aziz Ki, akiongoza kwa kufunga mabao akiwa nje ya eneo la hatari, kiungo wa Azam FC Feisal Salum ameonekana kuwa hatari kwa kufanya hivyo akiwa ndani ya boksi.
Aziz Ki, ambaye anaongoza kwa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao 10, anaongoza kwa kufunga mabao akiwa nje ya eneo la hatari ambapo mpaka sasa ana mabao manne akiyafunga nje ya boksi.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Burkina Faso anafuatiwa na kiungo wa Ihefu FC raia wa Togo, Marouf Tchakei mwenye mabao matatu, huku Clatous Chama, Mzambia anayeichezea Simba SC akishika nafasi ya tatu kwa kufunga mabao nje ya boksi, akifanya hivyo mara mbili, sambamba na wachezaji Velentino Mashaka na Tariq Seif, wote wa Geita Gold.
Kiungo Mshambuliaji Mtanzania, Fei Toto yeye anaongoza kwa kupachika mabao akiwa ndani ya boksi.
Amepachika mabao manane akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini pia mchezaji huyo ndiye anayemfuatia Aziz Ki kwa mabao mengi, akiwa ameshafikisha mabao tisa mpaka sasa.
Wachezaji wengine ambao wana mabao mengi waliyoyafunga wakiwa ndani ya eneo la hatari ni Jean Baleke ambaye alikuwa akiichezea Simba SC na sasa ameondoka kwenye kipindi cha uhamisho wa dirisha dogo akiwa amefunga mabao saba ndani ya boksi kwenye mabao nane aliyofunga kabla ya kuondoka nchini.
Baleke anaungana na Prince Dube wa Azam FC na Maxi Nzengeli wa Young Africans wenye idadi hiyo ya magoli ya ndani ya boksi.
Kiungo wa Simba SC Saido Ntibazonkiza, bado ameendelea kuwaburuza wenzake katika mabao ya penati kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa.
Kiungo huyo raia wa Burundi ana mabao manne aliyoyafunga kwa mikwaju ya penati huku takwimu zikionyesha hakuna hata mchezaji mmoja wa Ligi Kuu aliyefunga zaidi ya bao moja kwa njia hiyo.
Takwimu zinaonyesha wachezaji 13 wa Ligi Kuu wamefunga penati moja moja kila mmoja, ambao ni Febrice Ngoy na Derick Mulokozi wote wa Namungo, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki wa Young Africans, Jean Baleke wa Simba SC, Prince Dube na Feisal Salum wa Azam FC, Obrey Chirwa wa Kagera Sugar, Daniel Lyanga JKT Tanzania, Ibrahim Ajibu na Lucas Kikoti wote wa Coastal Union, Erick Okutu wa Tabora United na Jumanne El Fadhil wa Prisons.