Azam FC matajiri wa Dar balaa lao wanaliendeleza kutokana na kushinda kwenye mechi tano mfululizo ambazo ni dakika 450.
Ikumbukwe kwamba kasi ya Azam FC ilianza Novemba Mosi ubao wa Uwanja wa Lake Tanganyika ulisoma Mashujaa 0-3 Azam FC, Novemba 4 ubao wa Uwanja wa Highland Estate ulisoma Ihefu 1-3 Azam FC, Novemba 24 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 5-0 Mtibwa Sugar.
Kete ya kwanza kufungulia Desemba walikuwa nyumbani ubao wa Uwanja wa Azam Complex Desemba 7 ulisoma Azam FC 5-0 KMC ikiwa ni kete ya nne mfululizo kushinda na ile kete ya tano ilikuwa ni Desemba 11 ubao wa Azam Complex ulisoma Azam FC 2-1 JKT Tanzania.
Katika msako wa pointi 15 zote wamesepa nazo safu ya ushambuliaji ikitupia mabao 18 huku ukuta wao ukiruhusu mabao mawili pekee katika mechi tano ambazo ni dakika 450.
Kwenye mchezo wa juzi uliochezwa Uwanja wa Azam Complex mtambo wa kusoma ramani Idd Suleiman alianzia benchi na alipoingia alitibua mpango wa JKT Tanzania kuambulia pointi moja kwa kufunga bao la ushindi dakika ya 86.
Mchezo mwingine ambao Nado aliwahi kufunga bao la ushindi akitokea benchi ilikuwa dhidi ya Singida Fountain Gate alipomtungua Beno Kakolanya dakika ya 90 mwisho ubao ukawa Azam FC 2-1 Singida Fountain Gate.