Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajeti ya usajili Big Six si mchezo

Dszgfchgv Bajeti ya usajili Big Six si mchezo

Fri, 7 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ni wiki tu imebaki kabla ya dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kufunguliwa huko Ulaya, huku kila timu ikihaha kujiweka sawa kwa ajili ya kunasa saini za mastaa kadhaa watakaokwenda kufanya maboresho makubwa kwenye timu zao.

Klabu za Saudi Arabia zinatarajia kwenda kuvuruga hali ya hewa huko England, lakini kubwa linalojadiliwa kwa sasa ni kuhusu usajili utakaofanywa na klabu za Big Six kwenye dirisha hili. Manchester City, Arsenal, Liverpool, Manchester United, Tottenham na Chelsea zote zimetajwa kwamba zitakuwa bize kwenye dirisha hili kutafuta mastaa wapya wa kuja kuongeza nguvu kwenye vikosi vyao ili kufanya Ligi Kuu England ya msimu wa 2024-25 kwenda kuwa na ushindani mkali uwanjani.

1. Man City;

Ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu England, hivyo bila shaka kwenye dirisha hili timu hiyo itaingia sokoni kunasa nyota wapya ili kutengeza timu itakayokuwa na uwezo wa kutetea taji hilo. Man City imeripotiwa kutenga bajeti ya Pauni 200 milioni.

Mastaa ambao wapo kwenye rada za Man City ni kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, kiungo wa Bayern Munich, Joshua Kimmich na kiungo wa West Ham United, Lucas Paqueta ambaye hata hivyo yuko hatarini kufungiwa kwa kesi za kubeti. Kinachoonekana, Man City inasaka viungo tu, ambapo mastaa wengine inaowataka ni kiungo wa RB Leipzig, Dani Olmo na yule wa Benfica, Joao Neves na winga wa Real Madrid, Rodrygo.

2. Arsenal;

Ripoti zinafichua kwamba Arsenal itatenga kama bajeti ya dirisha lililopita, ambapo itaweka ubaoni Pauni 200 milioni kwa ajili ya kunasa mastaa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Kwenye rada za Arsenal, mchezaji anayepewa nafasi kubwa ya kunaswa kwenye dirisha hili ni straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko, ambapo kocha Mikel Arteta anatakiwa kukimbizana na muda hadi kufikia mwisho wa mwezi huu, awe amekamilisha dili la mchezaji huyo kama anamtaka. Mastaa wengine wanaosakwa huko Emirates ni kiungo wa Real Sociedad, Martin Zubimendi, kiungo wa Everton, Amadou Onana na mkali Bruno Guimaraes wa Newcastle na staa wa Aston Villa, Douglas Luiz. Inamtaka pia beki wa Ajax, Jorrel Hato.

3. Liverpool;

Miamba hiyo ya Anfield itaingia kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi chini ya kocha mpya, Arne Slot baada ya Jurgen Klopp kuondoka. Kijachoelezwa ni kwamba bajeti ya timu hiyo kwenye usajili ni Pauni 150 milioni, ambazo itatumia kuleta mastaa wapya Anfield.

Liverpool inasaka mastaa wengi, lakini chaguo lao la kwanza ni winga wa PSV, Johan Bakayoko huku ikimfukuzia pia staa wa Juventus, Federico Chiesa. Mastaa wengine wanaowindwa huko Anfield ni mkali wa Benfica, Antonio Silva, Goncalo Inacio wa Sporting CP, Piero Hincapie wa Bayer Leverkusen na Leny Yoro wa Lille. Liverpool itaingia sokoni kusaka kipa mpya pia.

4. Tottenham;

Haitacheza michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini itakuwapo kwenye Europa League. Bajeti ya usajili ya Tottenham itakuwa zaidi ya Pauni 50 milioni, lakini haitazidi Pauni 100 milioni. Imembakiza straika Timo Werner kikosini baada ya kucheza kwa mkopo kutoka RB Leipzig, lakini kwenye rada yao, wapo mastaa wengine inaowasaka, akiwamo Santiago Gimenez wa PSV, straika wa Brentford, Ivan Toney, fowadi wa Bournemouth, Dominic Solanke na yule wa Stuttgart, Serhou Guirassy na wa RB Leipzig, Luis Openda huku ikitambulisha wazi mpango wa Spurs kwenye usajili wa dirisha hili la majira ya kiangazi ni kunasa washambuliaji tu.

5. Chelsea;

Mauricio Pochettino ameondoka Chelsea na nafasi yake imechukuliwa na Enzo Maresca. Kwenye dirisha hili, Chelsea itafungulia mlango wa kutokea mastaa kibao, hivyo hilo litaifanya kuingia sokoni kunasa mastaa wengine, huku bajeti ikifanywa kuwa siri. Kuna mastaa wa maana ambao Chelsea inawataka, akiwamo straika wa Napoli, Victor Osimhen, anayeuzwa Pauni 115 milioni. Mastaa wengine wanaosakwa na miamba hiyo ya Stamford Bridge ni Benjamin Sesko, Viktor Gyokeres, Ivan Toney na Artem Dovbyk, jambo linalofanya bajeti ya usajili ya timu hiyo kutarajiwa kufika Pauni 200 milioni, huku mastaa wengine wanaosakwa ni beki Tosin Adarabioyo.

6. Man United;

Iliripotiwa kwamba Manchester United ina bajeti ya Pauni 35 milioni tu ya kusajili kwenye dirisha hili, hivyo itahitaji kufungulia mlango mastaa wake kadhaa ili kupata nafasi na pesa ya kuongeza wakali wapya. Man United inahitaji wachezaji wanne hadi watano katika dirisha hili la majira ya kiangazi, lakini mastaa inaowasaka haitanunua mchezaji mmoja kwa ada inayozidi Pauni 60 milioni. Kuna wachezaji wengi wataondoka na ndiyo maana timu hiyo inahusishwa na mpango wa kumsajili beki wa Everton, Jarrad Branthwaite, winga wa Crystal Palace, Michael Olise, huku wengine ni Max Kilman wa Wolves, Marc Guehi wa Palace, Jean-Clair Todibo wa Nice, mkali wa Juventus, Gleison Bremer na nyota wa Benfica, Antonio Silva pamoja na Leny Yoro wa Lille.

Chanzo: Mwanaspoti