Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'Bajeti Yanga inaakisi ukubwa'

Hersiiii Yangaaa Rais wa Yanga, Hersi Said

Tue, 27 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Klabu ya Yanga imetangaza mpango wake wa kutumia kitita cha Sh20 bilioni kama bajeti kwa ajili ya msimu ujao wa kimashindano.

Mpango huo uliowekwa wazi juzi kwenye mkutano mkuu wa klabu hiyo, unatajwa kuwa moja ya sababu za timu hiyo kufanya vizuri msimu ujao, ikiwa kutakuwa na uamuzi mzuri katika usajili na maandalizi ya timu.

Mkurugenzi wa Fedha wa Yanga, Sabri Sadick aliweka wazi kuwa timu hiyo ina Sh14.8 bilioni ilizovuna msimu huu kupitia vyanzo vyake vya mapato, hivyo itahakikisha inapata nyongeza ya Sh6 bilioni ili kufikia lengo.

"Katika vyanzo vyetu vya mapato tuna Sh14.8 bilioni, hivyo tuna upungufu wa Sh6 bilioni ingawa tunaamini tutafanyia kazi kwa haraka na kushirikiana na wadhamini wetu ili kufikia malengo."

Aidha Sabri aliongeza kiasi hicho kilichotengwa kwa msimu wa 2023/24 ni zaidi ya msimu uliopita kwani timu hiyo ilitumia Sh17.8 bilioni huku matumizi kwa msimu mzima yakiwa ni Sh17.3 bilioni.

"Hadi sasa kiasi cha fedha zilizobaki kwa msimu uliomalizika ni Sh581 milioni, hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa ili kuongeza ufanisi zaidi kwa timu yetu msimu ujao,"alisema Sabri katika mkutano huo.

Bajeti hiyo inakuwa kubwa zaidi kwa klabu ya soka nchini kuwahi kuifikiria katika mwaka mmoja wa kimashindano tangu kuwa na maendeleo ya soka nchini, ikiwa ni ongezeko la Sh2.7 bilioni.

Akizungumzia hatua hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, ambaye pia ni nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema hakushangazwa na bajeti hiyo kutokana na ukubwa wa Yanga.

"Bajeti inaongezeka kutokana na mahitaji ya timu, sasa ukiiangalia Yanga ilipoishia msimu uliopita unaona kabisa ni lazima kutakuwa na ongezeko ambalo linalenga manufaa huko mbeleni," alisema Mayay.

Kwa upande wake, mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Sekilojo Chambua alisema kuongezeka kwa bajeti ni kuonyesha jinsi gani viongozi wanahitaji kuendelea kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

"Yanga ilichukua mataji yote ya ndani msimu ulioisha na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho na msimu ujao inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo lazima kutakuwa na mambo mengi," alisema.

Katika matumizi ya msimu uliopita Sabri alisema fedha hizo zimetokana na udhamini, kiingilio cha milangoni, ada za wanachama, zawadi ya ushindi, mauzo ya wachezaji, faida ya jezi, mikopo na mapato mengine.

Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na wanachama 531, alisema malengo yao makubwa kama viongozi ni kuona Yanga inazidi kupiga hatua ndani na nje ya nchi.

Mbali na agenda mbalimbali zilizojadiliwa ila pia timu hiyo ilitumia mkutano huo kumtambulisha kocha mkuu, Miguel Angel Gamondi aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyemaliza mkataba wake.

Tukio hilo ni muendelezo kwa Yanga kutoa 'Surprise' (mshangao) kwa wanachama wake, kwani kwenye uchaguzi mkuu wa Julai, mwaka jana, ilimtambulisha kiungo, Gael Bigirimana aliyeichezea Newcastle ya England.

Bajeti hiyo ilipitishwa juzi katika mkutano mkuu wa mwaka wa timu hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere (JNICC).

Mkutano huo ni wa kwanza kwa Yanga tangu uwaingize madarakani rais wa klabu hiyo, Hersi Said, Makamu wa Rais, Arafat Haji na wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa Julai mwaka jana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: