Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bajana agoma kubebwa

Bajana X Amrabat Sospeter Bajana

Sat, 20 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Siku chache baada ya rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, kusema hawatopunguza wachezaji 12 wa kigeni kama ambavyo ilipendekezwa na baadhi ya wadau wa soka kwenye maboresho ya kanuni ya msimu ujao, mchezaji wa Azam FC, Sospeter Bajana, amewaibukia na kuwataka wachezaji wenzake wa Kitanzania kupambania namba na si kutegemea kanuni kwani itawashushia hadhi.

Akizungumza akiwa nchini Morocco ambako kikosi cha Azam FC kimeweka kambi kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, Bajana alisema wachezaji wa Kitanzania kama watajitambua, wanaweza kupata namba kwenye kikosi chochote kile nchini na kuwapiku wanaotoka nje.

Alisema atafurahi kuona mchezaji wa Kitanzania anacheza kutokana na kiwango chake anachokionyesha uwanjani na kukubalika na kocha, badala ya kupangwa kwa sababu ya kubebwa na kanuni.

"Mjadala nimeusikia, mimi sidhani kama sisi wenyewe wachezaji linatusumbua sana, ni kiasi cha mchezaji mwenyewe kujitambua kujua nini anafanya uwanjani, tukiweza kupambana na kuwaweka nje wachezaji wa kigeni, itatupandisha thamani, mfano akiletwa mchezaji ambaye kiwango kiko juu na wewe inabidi upandishe kiwango chako," alisema kiungo huyo mkabaji.

Aliwaasa wachezaji wenzake kwamba kupambana kutawasaidia wao wenyewe na familia zao na si kwa ajili ya klabu pekee.

"Naawambia tu wachezaji wenzangu, akiletwa mchezaji kutoka nje ni lazima apambane kuwania nafasi kwa sababu hiyo itamsaidia yeye mwenyewe kwanza kuborosha kiwango chake ili hata klabu za nje ziweze kummmezea mate.

"Ataisaidia klabu yake kupata ushindi, pia atalisaidia taifa kwani kiwango chake kitamfanya kuitwa Taifa Stars na atakuwa ni mchezaji aliyeitwa kwa ubora, si kwa sababu anapewa nafasi ya kucheza kwa kanuni," alipigilia msumari.

Naye winga wa timu hiyo raia wa Gambia, Gibril Sillah, aliwataka wachezaji wa Kitanzania kutowaogopa, kwani hata wao wanalazimika kupambana kupata namba kwa kuwa wanatoka nje ya nchi na kukuta kuna wachezaji wengi wazawa ndani ya kikosi, hivyo nao wanakuwa na hofu kama hiyo, lakini hawalalamiki zaidi ya kupambana.

"Kwangu mimi nawashauri wachezaji wa Tanzania, mfano Azam ina wachezaji 12 wa kigeni, waliobaki wote ni wazawa, sasa kama unataka kucheza basi unapaswa kufanya kazi, na hata sisi wachezaji wa kigeni tunafanya kazi sana, maana ukiona mchezaji wa Kitanzania anakuweka benchi, basi lazima uwe na tahadhari kwani unaweza kuondoka muda wowote, hivyo ni lazima upambanie nafasi yako," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live