Taifa Stars jana usiku ilipasuka mabao 2-0 kutoka kwa Morocco katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 na baada ya mchezo huo, kiungo wa Stars, Sospeter Bajana alifuatwa na kiungo nyota wa Morocco anayekipiga Manchester United, Sofyan Amrabat na kuteta kabla ya kubadilishana jezi.
Mwanaspoti lilimsaka Bajana anayekipiga Azam FC na aliyeupiga mwingi kwenye mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa na kueleza nyota huyo wa Manchester United alimfuata na kuomba kubadilishana naye jezi, huku akimsifia kwa kiwango alichokionyesha kwenye pambano hilo la Kundi D.
"Sikutarajia kama Amrabat angeniomba jezi, lakini alinifuata mwenyewe na kupiga naye stori mbili tatu akinisifia kabla ya kubadilisha naye jezi. Aliniambia mimi ni miongoni mwa wachezaji wazuri," alisema Bajana na kuongeza, amechukulia jambo kwa ukubwa na amejifunza kitu katika maisha yake ya soka.
Alisema kauli ya nyota huyo wa Morocco imemuongezea morali wa kuendelea kupambana kutokana na mchezaji huyo mkubwa kumfuata kwani ameona ni jambo la thamani.
"Hakuwa na maneno mengi, lakini jambo aliloniambia ni; wewe ni kiungo mzuri sana, nilichukulia jambo lile thamani kubwa sana kwenye kazi yangu kupongezwa na mchezaji kama yule wa daraja la juu," alisema Bajana mwenye mabao mawili katika Ligi Kuu kwa sasa akiwa na timu ya Azam inayoshika nafasi ya pili.