Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Badru: Chama, Luis ni zaidi ya majembe

Badru Pic 1 Data Badru: Chama, Luis ni zaidi ya majembe

Tue, 30 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

ALIIPIGANIA ndoto yake bila kujali ugumu wa mazingira, nchi ngeni lakini akajiona ni shujaa aliyetayari kuanza vita ya maisha, unajua ni nani huyo! Ni kocha wa Gwambina, Mohammed Badru aliyeishi England zaidi ya miaka 10 bila kukanyaga ardhi ya Tanzania.

Mwanaspoti lilifanya naye mahojiano maalumu ambapo alifichua mambo mengi mazito, ikiwemo maisha yake ya England alianzia kusafisha nyumba za watu, aliendesha taksi hadi kusomea ukocha, ngazi ya tatu ya Fifa, huku akiwataja nyota wa Simba, Luis Miquissone, Clatous Chama na Bernard Morrison kuwa ni majembe kwelikweli na miongoni mwa wachezaji wanaoisuuza roho yake nchini.

Tofauti na muonekano wake wa upole unaoweza kukudanganya na kumuona ni wa kawaida, ukweli ni kwamba ukikaa na Badru na kujipa utulivu wa sikio, unagundua ana madini yanayoweza kuwabadilisha wachezaji Tanzania, mazito aliyopitia, ushujaa wa kuamini katika ndoto zake.

“Mwanaume hujiulizi mara mbilimbili kufanya uamuzi, ndio maana nilianza na kazi za kufanya usafi majumba ya watu hadi kusomea ukocha na mastaa wakubwa Ulaya,” anasema.

ILIKUAJE AKAENDA ENGLAND

Sababu ambayo ilimfanya kuondoka visiwani, Zanzibar kwenda England huku akifichua kwamba maamuzi hayo hakuwashirikisha ndugu zake zaidi ya marafiki zake ambao nao walikuwa na mawazo sawa na yake, hawakuona umuhimu wa kuendelea na shule.

“Niliondoka nikiwa mdogo, nakumbuka nilikuwa na miaka 19, nilirudi Tanzania nikiwa na miaka 30 unaweza kuona kuwa nilipambana ugenini kwa zaidi ya miaka 10. Unajua mawazo ya vijana wa Zanzibar kwa kizazi chetu yalikuwa ni kusafiri kwenda nje kutafuta maisha, nikiwa Sekondari na wenzangu tulianza mipango,”

“Nakumbuka tuliondoka Tanzania mwaka 1993. Mipango ya kuondoka ilikuwa kama utani kwani nilianza kujiongeza kwa kufanya biashara ndogo ndogo nikitoka shule, nilipambana na kupata kiasi ambacho niliona kimetosha kwa ajili ya nauli ya kwenda England na kukaa hoteli,”

“Niliandaa kitu kama Dolla 1,200 sawa na Sh 2.7 milioni kilikuwa kiasi kingi na kwa wakati huo hapakuwa na mambo ya visa wala nini kwa hiyo ilikuwa rahisi kwangu na marafiki zangu kuingia nchini humo, nyumbani hawakuwa wanajua juu ya mpango huo,”

“Kipindi hicho kaka yangu (Hafidhi), alikuwa anatamba kwa sababu alikuwa kocha mkubwa Tanzania naye nilimficha. Nakumbuka ile siku ambayo nimeshakata tiketi nilikosa usingizi maana mawazo yangu yote yalikuwa Ulaya,” anasema.

Baada ya kukucha akiwa macho, Badru anasema hakutaka kupandia ndege visiwani humo hivyo alivuka bahari na kuja Bara ili apandie jijini Dar es Salaam sehemu ambayo aliamini hata iwaje hakuna ndugu yake ambaye anaweza kuwepo kwa ajili ya kumzuia.

Badru anasema; “Nilicheza kwa akili ili mpango wangu usikwamishwe na mtu yeyote, maana kuna watu niliwaonyesha tiketi yangu kuwa siku sio nyingi naondoka Zanzibar na kwenda Ulaya kutafuta maisha, kwa bahati nzuri niliondoka Tanzania bila kizuizi chochote huku nikiwaacha nyumbani bila taarifa yoyote juu ya safari hiyo.”

MAISHA YA ENGLAND

Baada ya kusepa Tanzania, Badru anasema ile siku ya kwanza tu anatua jijini London, alikuwa akishangaa huku changamoto kubwa sasa ikiwa kwenye lugha maana aliondoka Tanzania akiwa kidato cha pili na masuala ya shule na yeye vilikuwa vitu viwili tofauti.

“Sijui ingekuwaje maana sidhani kama ningeweza kutoka uwanja wa ndege maana sikuwa najua chochote na lugha ilikuwa changamoto, nilipokewa vizuri na yule Bwana na kunipeka moja kwa moja Hotelini ambako nilikuwa napata kila kitu kama ambavyo nilikuwa natarajia, hapo nilikuwa nimebaki mfukoni na kiasi kidogo sana,”

“Nikiwa nimeanza maisha mapya ya kukaa Hotelini jijini London, ndipo nikawa nazurula mtaani ili kusoma mitaa, ndipo nilipoona kwenye duka moja wamebandika tangazo la kazi, ni kweli lugha ilikuwa changamoto ila sikuwa sifuri kabisa kichwani nilikuwa nikiibiaibia kwa kujua baadhi ya maneno ya Kiingereza,”

“Nilitumia fursa hiyo na kupata kazi, kipindi hicho hapakuwa na mambo ya kutaka sijui vibali vyako na mambo mengine maana ilikuwa ni kazi ya kutumia nguvu, kwangu sikuwa na chagua cha kufanya kila kazi nilisema nayo na mwisho wa siku mambo yakaninyokea, kwa sababu nilikuwa nimeshakuwa mwenyeji nilipate sehemu nyingine ya kaa,” anasema.

Badru alipata mke akiwa England na kushirikiana naye kwenye kutafuta maisha, marafiki zake wapo ambao walizolea wanawake wa Kizungu lakini yeye hakutaka kuondoka kwenye uasili wake,”Mke wangu ni Mtanzania kabisa, nilikutana naye kwenye mazingira ya kazi.”

ALISOMA NA LEDLEY KING

Badru alinufaika na nafasi za kijamii ambazo kwa wenzetu huwa zinatokea, alianza kujiendeleza kielemu kwa kusoma ya watu wazima na baada ya hapo kwa sababu alikuwa anakaa London karibu na Tottenham Hotspur FC akapata shavu lingine.

Spurs ilimsomesha chuo ambako alisomea elimu ya michezo na kupata diploma, akiwa anafanyia kazi kwa vitendo kile alichosomea ndipo walipoona anaweza kuwa kocha mzuri, alipelekwa kusomea ukocha na huko ndipo alipoonana na Ledley King.

“Nadhani kwa watu ambao wanafuatilia mpira wa England hili jina sio geni kwao, kwa sababu alicheza Ligi hiyo akiwa na Tottenham, jamaa kuna matatizo alikuwa nayo hivyo yalimfanya kuachana na soka akiwa na umri mdogo,”

“Tulisomea wote ukocha na kumaliza pamoja, ni mtu poa sana na mwenye upendo, pengine labda ni kwa sababu ya kuwa asili yake ni Afrika,” anasema.

MAHUSIANO YALIOMUUMIZA

Ukiachana na mke wake wa kwanza aliyemuoa mwaka 1999 huku nchini England ambaye ni Mwafrika mwenzake, anasema baada ya kurejea Tanzania alioa mke wa pili, kutokana na kisa kizito kilichomlazimu kufanya maamuzi hayo.

Anaficha jina la kambi aliyokutana na mwanamke wa pili aliyemuoa kwamba, alishangazwa na uhodari wa kuulizwa maswali ambao hakuwahi kukumbana nayo hapo awali, baada ya darasa aliombwa akutane naye kwa mazungumzo binafsi.

“Nilikubali kuzungumza naye binafsi ambayo hayakuhusiana na mahusiano kabisa, niliondoka na kuendelea na maisha mengine, kiukweli sikuwa na wazo la kuoa kabisa, kwani tayari nilikuwa na familia niliyoiacha England,” anasema na kuongeza kuwa;

“Baada ya kupita muda mrefu, kuna rafiki yangu mmoja alikutana naye akiwa amebadilika na kuwa mcha Mungu mzuri, akaniambia kwanini usimuoe ili asije akarejea kwenye madawa na kwa kuwa ulimsaidia kumjenga hadi kuwa alivyo, nikatafuta namba yake ya simu nikampigia nahitaji kukuoa, alikataa na kwamba wanaume wote ni walewale, nikagundua kwamba aliwahi kuolewa, nikamuomba nikutane naye,” anasema.

Anasema baada ya kukutana naye ndipo alijua mazito zaidi kuhusu maisha yake.

AMETOKEA FAMILIA YA MPIRA

Mzanzibar huyo anasema ametokea familia ya mpira hivyo kuwa kocha haikuwa bahati mbaya licha ya kutocheza mpira ngazi yoyote kubwa ya ushindani.

“Baba yangu alikuwa kiongozi mmoja mkubwa tu kwenye Chama cha Mpira cha Zanzibar, sikumbuki nafasi yake lakini nilikuwa nikimwona akija Bara kwenye vikao mbalimbali vya FAT kabla ya jina kubadilika la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).”

“Kijiti cha Baba alikichukua Kaka yangu na kufundisha soka kwenye ngazi kubwa ya taifa, nadhani wengi wanamfahamu Hafidhi Badru aliifundisha Taifa Stars pamoja na timu ya taifa la Zanzibar, sasa hivi nimempokea na ninaimani kuwa nitafanya makubwa kwa ujuzi ambao nimeupata England,” anasema kocha huyo.

KUTUA GWAMBINA

Baada ya kuamua kurejea Tanzania, Badru anasema alipenda atoe mchango wake kwa maendeleo ya soka la nyumbani licha ya kufundisha soka akiwa England kwenye timu mbalimbali za vijana ndipo alipopata kibarua cha kuinoa Malindi.

“Nilikuwa nikiifundisha Malindi ya Ligi Kuu Zanzibar kabla ya kupata nafasi Gwambina, viongozi walivutiwa na uwezo wangu ndio maana wakanipa timu kwa sharti moja tu, kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu maana mwenendo haukuwa mzuri,”

KILICHOMKUMBA SAMATTA ENGLAND

Akiwa England, Badru alimshuhudia Samatta akicheza Ligi hiyo na alifurahishwa mno kutua kwake Aston Villa, aliamini kuwa nahodha huyo wa Stars anaweza kufanya makubwa baada ya kutamba kwa kipindi kirefu akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji.

“Makocha wengi England ni wepesi mno kumsoma mchezaji ndicho kilichotokea kwa Samatta, alikuwa mzuri mwanzoni lakini baada ya kusomwa alishindwa kufanya maajabu tena, kazi ya mshambuliaji ni moja tu kufunga kama hufungi ni rahisi kuondolewa kikosini,”

“Halafu inaonekana alisajiliwa kama mbadala tu hakuwa chaguo la kwanza ndio maana baada ya kufeli hapakuwa na muda wa kumuangalia msimu uliofuata,” anasema.

SIMBA/YANGA

Anasema Simba kwasasa ipo kiwango cha juu, akitofautisha na Yanga anayoona inatakiwa kujipanga ili kuwa kwenye ushindani unaolingana na uzito wa klabu hiyo kuwa kongwe na utajiri wa mashabiki.

“Simba imejipanga kila idara, ina kikosi imara kinachoanza na kinachokaa benchi, ndio maana wanacheza soka la uhakika uwanjani, kipindi hiki sijaona mpinzani wake ni kama ilivyokuwa Yanga miaka kadha iliyopita ilikuwa vizuri zaidi ndio maana ilifanikiwa kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo,”anasema.

Anashauri nini wafanye Simba, mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika, wakikutana na timu inayocheza aina yao;

LUIS NA CHAMA

Anawataja mastaa anaowakubali Ligi Kuu Bara ambao anaona wana vipaji vya hali ya juu na wanacheza soka linaloburudisha kuwa ni Luis Miquissone, Clatous Chama na Benard Morrison kutoka Simba.

“Kwa namna soka la Uingereza lilivyo na kwa muda niliokaa, ninaweza kuwa na ujasiri wa kumwambia wakala wa nje njoo umuone Luis, najua hatapoteza muda wake, anaweza kucheza nchi yoyote ni vitu vichache anatakiwa kurekebishwa ili aweze kushangaza dunia,” anasena na anaongeza kuwa;

“Lakini Morrison aliyekuwa Yanga alifanya mengi kwasababu walimuacha huru ili kuonyesha hazina zilizopo miguuni kwake, lakini Simba anachezeshwa kwa maelekezo ndio maana anonekana kama uwezo amepungua, Chama sio mchezaji mwenye mikimiki ila ana akili ya nini afanye na kwa wakati gani,” anasema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz