Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bado hatuamini soka letu limepiga hatua kubwa Afrika?

Yanga, Namungo Bado hatuamini soka letu limepiga hatua kubwa Afrika?

Mon, 19 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Soka letu limepiga hatua sana hasa katika ngazi ya klabu. Inafurahisha kuziona Simba na Yanga kwenye hatua ya makundi ya michuano ya CAF. Tumepiga hatua.

Ilikuwa nadra sana kuziona timu za Tanzania katika hatua hii ya michuano ya CAF. Mfano mzuri ni pale Yanga ilipokaa miaka 18 bila kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF.

Tangu walipofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1998, walifuzu hatua kama hiyo ya Kombe la Shirikisho 2016. Ni muda mrefu sana ulipita.

Lakini ndani ya miaka hii sita, Yanga imefuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya tatu sasa. Ni hatua kubwa sana. Wanastahili pongezi kwa kuanza kuona nuru.

Vivyo hivyo kwa Simba. Iliwachukua miaka 15 tangu walipofuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuzu kwa mara nyingine tena. Walisubiri kuanzia 2003 hadi 2018.

Lakini katika miaka hii minne wamefika hatua ya robo fainali ya michuano ya CAF mara tatu. Ni mwendelezo mzuri sana. Haikuwa mazoea kwa timu zetu kufanya hivyo.

Tulitamani siku moja timu zetu ziwe zinafuzu hatua ya makundi ya mashindano ya CAF mara kwa mara. Hatimaye ndoto inaelekea kuwa kweli.

Ni katika nyakati hizi pia Namungo nayo ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Inapendeza sana.

Japo watu wengi kwa sababu zao mbalimbali huwa hawazungumzi haya kama mafanikio. Wanaona kama ni jambo la kawaida, lakini ukweli ni kwamba hii ni hatua kubwa sana.

Ndio sababu hata kwenye CAF sasa tumepata uwakilishi wa timu nne katika mashindano yao. Ni nchi 12 tu Afrika zinaingiza timu nne. Tupo katika dunia yetu.

Ni kweli kuwa itachukua muda mrefu kuweza kutwaa ubingwa wa Afrika, lakini kufika makundi au robo fainali kwa sasa ni mafanikio makubwa.

Mafanikio haya makubwa yametokana na uwekezaji wa matajiri wakubwa katika soka letu. Lazima tukubali kuwa Mohamed ‘MO’ Dewji amebadili kila kitu pale Simba.

Aliikuta timu ikiwa haina ushindani. Akaweka pesa nyingi. Wakafanya usajili wa wachezaji wakubwa. Wakaweka maisha mazuri kambini na posho nyingi.

Akaimarisha benchi la ufundi. Akaimarisha ofisi na watendaji wake. Simba ikawa timu kubwa ndani na nje ya uwanja.

Simba ikawa inasafiri nchi zote za Afrika bila tabu. Ikaweza kuvuka vikwazo na fitna zote za wageni. Ndio sababu Simba leo inaweza kushinda sehemu yoyote.

Hapa ndipo ushindani halisi wa Simba ulipoanzia. Wamekuwa wakubwa Afrika.

Yanga nao uwekezaji wa GSM umeanza kuwalipa. Baada ya miaka mitatu tu wamefika hatua ya makundi kwenye Kombe la Shirikisho. Haijaja bahati mbaya.

GSM aliikuta Yanga katika maisha magumu. Haikuwa na uwezo wa kusajili wachezaji mahiri. Haikuwa na kambi ya kueleweka wala uhakika wa kulipa mishahara.

Akabadili kila kitu. Leo Yanga inafanya usajili mkubwa.

Ina kambi nzuri pale Avic Town na inalipa mishahara kwa wakati. Hapa ndipo ushindani mkubwa ulipoanzia.

Fikiria namna ambavyo Yanga walikwenda pale Tunisia. Walitumia fedha nyingi katika usafiri na kambi. Wakaenda kuitoa Club Africain palepale kwao. Inafurahisha sana.

Njoo huku kwa Namungo. Wale matajiri wa pale Ruangwa kwa usimamizi wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wameifanya kuwa timu kubwa.

Leo pale Ruangwa wana uwanja wa kisasa wa mpira. Mechi zinachezwa hadi usiku. Ni jambo ambalo lilionekana kama ndoto, lakini leo imewezekana.

Namungo inachukua makocha wakubwa na wachezaji mahiri pia. Ni maendeleo makubwa katika soka letu.

Mji mdogo kama Ruangwa kuwa na timu imara na uwanja wa kisasa wa soka sio jambo dogo.

Kuna ule uwekezaji mwingine pale Chamazi. Hawa wana shida zao lakini ni uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na timu ya soka nchini.

Ipo siku Azam itakaa sawa pia na kuweza kushindana Afrika. Wana kila kitu cha kufanya hivyo. Pengine wanakosa tu watu sahihi wa kuwaonyesha njia za kupita.

Ila kama ni pesa, Azam FC wanazo kuliko timu yoyote nchini. Wana basi kali kuliko timu yoyote Afrika Mashariki. Wana uwanja wa kisasa. Mungu awape nini tena?

Chanzo: Mwanaspoti