Mzee Abdallah Hamad, ambaye ni baba mzazi wa beki wa Kati wa Yanga, Ibrahim Hamad Abdullah Bacca amesema kuwa mwanaye huyo aliwahi kuwekwa lupango na KMKM baada ya kutoroka na kwenda kusaini katika Klabu ya Polisi Tanzania bila ridhaa ya timu yake ya KMKM FC.
Ikumbukwe kuwa, Bacca ni mwajiriwa wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar ambapo alikuwa akiitumikia timu ya kikosi hicho kama mwajiriwa wa jeshi na mchezaji wa timu ya soka ya KMKM kabla ya kujiunga na Yanga.
"Nilimwambia cha kwanza usiache kazi na viongozi wake wa KMKM walikuwa wakiniita mara kwa mara sababu zilikuja timu nyingi, Namungo, KMC, Geita zilikuwa timu kama nne hivi lakini KMKM wakasema hapana, huyu sio mtu wa kwenda Namungo wala KMC, wakamwambia wewe vuta subira utaenda tu.
"Baadaye yeye na Abdulmarick Zacharia wkaenda kusaini Polisi Tanzania, alijiiba kule akatoroka kwenda kusaini. Kwa hiyo KMKM wakaniita, wakaniambia Ibra kafanya nini? Nikamuita. Mimi nilikuwa najua lakini baadaye nikamtuliza.
Baada ya kurudi hapa, KMKM walimweka ndani kama tatu, nikaitwa tukaenda kuzungumza nao, wakamwambia wewe tulia, sisi wenyewe itafika pahala hatuwezi kukuzuia, utaenda zako.
Alipokuja Injinia Hersi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, vijana wa Kizanzibar, wakeleketwa, wakaenda mpaka kwa Injinia kumwambia tuchukulie Ibrahim Bacca, uzuri nay eye alikuwa ameshaona uwezo wake, ikawa rahisi. Uzuri hata viongozi wa KMKM hawakuleta tabu.
"Kwa sasa Ibrahim bado ni mwajiriwa wa Serikali, hajaacha kazi, amepewa kibali maalum, siku akimaliza atarudi kwenye kazi yake," amesema Mzee Hamad.