Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bacca anavyoipiga tafu KMKM

Bacca X KMKM Beki wa Yanga SC, Ibrahim Hamad ‘Bacca’

Mon, 3 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Beki wa Yanga SC, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaokumbukwa zaidi na KMKM ya Zanzibar kutokana na aliyowahi kuyafanya ndani ya timu hiyo sambamba na yale anayoendelea kuyafanya.

Bacca ambaye alijiunga na Yanga Januari 2022 akitokea KMKM, bado moyo wake upo klabuni hapo kwani ndiyo sehemu ambayo ilikuwa kama daraja kwake la mafanikio aliyonayo hivi sasa.

Kocha Mkuu wa KMKM, Ame Msimu, amefichua hilo baada ya kufanya mahojiano maalum na Mwanaspoti huku akianza kwa kumzunguzia beki huyo namna kiwango chake kilivyo.

“Bacca nampongeza kwa kiwango chake anachokionyesha na muendelezo wake, ni mchezaji mzuri mwenye tabia nzuri.

“Ibrahim Bacca ni mchezaji mmoja ambaye alikuwa mwandamizi, alikuwa ni mfano kwa wenzake, alikuwa anafanya yale yote yaliyokuwa yanahitajika kwenye timu na kuwa msaada.

“Yote kwa yote imekuja fursa hii na kile anachokionyesha naamini atafika mbali kwa namna alipotoka na anavyoendelea. Lakini wapo vijana wengi ambao hawajapata fursa kama yake tunao,” amesema Kocha Msimu.

Bacca ambaye wengi wamekuwa wakimfahamu kama askari huku baadhi yao wakiwa hawana uhakika na hicho wanachokisema, Kocha Msimu anaweka wazi jambo hilo akisema: “Bacca ni askari na cheo alichonacho ni cha koplo.”

ALIVYOJIUNGA NA YANGA WAKATI BADO NI ASKARI

Licha ya kwamba Bacca amejiunga na Yanga, lakini bado beki huyo ni askari katika kikosi cha KMKM. Inaelezwa kwamba, uhamisho wake haukuwa na tatizo na wala haukumzuia kuondoka KMKM na kutua Yanga kwani sheria za klabu hiyo zilimbeba.

“Uhamisho wake kutoka KMKM kwenda Yanga ni wakuu wenyewe walikaa na kuona kwa sababu yeye ni mwanamichezo na fursa ilivyokuja ilikuwa ni rahisi kabisa kukubaliana nayo. Wakuu walipokaa wakaona acha aende kuitumikia Yanga huku akiwa bado askari kwani ni vitu vilivyokubalika na mpaka leo yeye ni askari licha ya kwamba anacheza katika timu ya uraia.

KUMBE SIO KWA BACCA PEKEE

“Hii ipo siyo kwa Bacca tu, ishawahi kutokea huko nyuma kwa Mudathir golikipa wetu na itaendelea kutokea kwa wengine. Bacca ametoa fursa kwa hiyo wapo wachezaji wengi ambao nao wakipata fursa nafasi ipo ya kuruhusiwa.

SAPOTI YAKE KWA TIMU

“Ibrahim Bacca anatoa sapoti kubwa sana kwa KMKM, pindi anapopata mapumziko basi anakuja kufanya mazoezi na wenzake, anatoa hamasa kwenye timu, morali na kusapoti, kuna kipindi anawaahidi wachezaji wakishinda anatoa bonasi.

“Hiki ni kitu cha kuigwa na anafanya mara kwa mara kadiri iwezekanavyo, amekuwa akitoa sapoti kwa vijana wenzake na kila kitu kinakwenda vizuri,” alisema kocha huyo.

Rekodi zinaonyesha kwamba, Bacca ambaye alitua Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu wa 2021-2022, amekuwa chachu kubwa ya mafanikio kwa timu hiyo akicheza beki wa kati sambamba na Dickson Job na Bakari Mwamnyeto.

Mpaka sasa beki huyo ndani ya Yanga ameshinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na mawili ya Kombe la FA, huku akiwemo kwenye kikosi hicho kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.

Bacca alianza kucheza soka la ushindani katika timu ya Jang'ombe Boys 2017–2019, kisha Malindi 2019–2021, ndipo akajiunga na KMKM 2021–2022 msimu ambao alifanikiwa kushinda ubingwa wa Lig Kuu Zanzibar, kabla ya kutua Yanga 2022.

Chini ya Kocha Nasreddine Nabi kabla ya ujio wa Migule Gamondi, Bacca amekuwa beki muhimu wa eneo la ulinzi la kati ndani ya Yanga, huku mafanikio ya klabu hiyo kwa misimu mitatu mfululizo yeye akiwa miongoni mwa waliotoa mchango mkubwa sana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: