Mshambuliaji wa Mashujaa FC, Adam Adam amesema Ligi Kuu Tanzania Bara ina mabeki wengi wa kati lakini beki wa Young Africans, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ ndiye anayempa wakati mgumu wanapokutana uwanjani.
Adam amesema kuwa timu kubwa zinaenda mbali kusajili lakini zikitulia hapa nyumbani kuna wachezaji wengi wazuri na viwango vyao vinalingana na hao wa nje ya nchi, akimtolea mfano Bacca ambaye ndio muhimili wa safu ya ulinzi ya Young Africans.
“Bacca ni mchezaji mzuri na mtulivu anayeweza kukabiliana na mshambuliaji wa aina yoyote ile ndio maana hata mimi ninapokutana naye huwa Napata wakati mgumu kutokana na ubora wake.
“Upande wa nyota chipukizi anayenifurahisha ni Clement Mzize kwa staili yake ya uchezaji, ni mchezaji mwenye kipaji cha kipekee ambaye kama akiendelea hivi atafika mbali,” amesema Adam.
Katika hatua nyingine Adam amesema kuwa katika mchezo ujao dhidi ya Simba SC, wao hawaangalii ukubwa wao wanachoangalia ni kucheza mpira.
“Tukikutana na Simba SC tutawaheshimu ni timu kubwa lakini haifanyi tuwe wanyonge kwa sababu tuliwahi kukutana na kuchukua pointi tukiwa na timu nyingine ingawa msimu huu ligi ni ngumu kila timu inasaka pointi ili ikae katika nafasi za juu.”