Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bacca adokeza siri ya ukuta imara Yanga

Bacca Pic Beki wa kati wa Yanga Ibrahim Abdullah ‘Bacca’

Thu, 27 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Beki wa kati wa Yanga, Ibrahim Abdullah 'Bacca' amesema ubora wa safu hiyo ndio siri ya mafanikio huku akimtaja Yanick Bangala kuwa ndiye kiongozi, lakini akicheza namba sita.

Yanga inayoundwa na ukuta wa Joyce Lomalisa, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Bacca, Djuma Shaban, Kibwana Shomari na Yanick Bangala imeruhusu mabao 13.

Akizungumza Bacca alisema anafurahi kucheza na mabeki wote waliopo Yanga kutokana na kila mmoja kuwa na aina yake ya uchezaji huku akisisitiza anafurahi zaidi akicheza na Bangala kama namba sita.

"Mabeki wote nimepata nafasi ya kucheza nao wana uwezo na ni viongozi wazuri kiwanjani lakini nafurahi zaidi nikicheza na beki mwingine kati na Bangala akawa juu kama namba sita ni mtu makini sana na anapenda kuzungumza mimi namuita beki kiongozi;

"Mkicheza uwanjani kwa kukumbushana majukumu mchezo wa mpira ni mwepesi na makosa mengi yanapungua tuna nahodha Mwamnyeto anazungumza ana kila sifa ya kuwa kiongozi lakini kuna Bangala hapendi timu ifungwe kizembe," alisema.

Bacca alisema uimara wa safu yao ya ulinzi unajengwa na kuelewana vizuri na kukumbushana majukumu wawapo uwanjani huku akisisitiza kila mchezaji aliyepo kwenye safu hiyo ana ubora wake.

Alisema umuhimu wa Bangala uwanjani unafahamika ni mchezaji ambaye anaweza kutumika sehemu nyingi uwanjani na anafanya vizuri kila anapopangwa hilo pia linamfanya aweze kujifunza mengi kutoka kwake.

"Siwezi kutaja sifa za kila mchezaji ila kile kinachoonekana uwanjani kinatokana na kuaminiana na kupeana maelekezo ili kila mmoja aweze kufanya kwa ubora na timu ipate matokeo mazuri." alisema.

Hivi karibuni rais wa Yanga, Hersi Said amesema kiwango ambacho anakionyesha Bacca kimewashawishi wapo kwenye mchakato wa kuboresha maslahi yake.

Hersi aliongea hayo na moja ya chombo cha habari baada ya mchezo wao wa robo fainali ya kombe Shirikisho dhidi ya Rivers United huku ikishinda 2-0.

Hersi alisema Bacca ni mmoja ya mabeki bora nchini Tanzania na ana utulivu anapokuwa uwanjani, pia anatumia miguu yote miwili kwenye kucheza mpira wameona umuhimu wa kukaa naye na kumboresha maslahi yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live