Mlinzi wa timu ya soka ya Tanzania 'Taifa Stars', Ibrahim Hamad 'Bacca' amesema siri yake kubwa ya kucheza vyema katika michuano ya AFCON mwaka huu ilikuwa ni kujituma kwa nguvu zote.
Mlinzi huyo wa Yanga amesema hayo mara aliporejea alfajiri ya leo na Kikosi cha Taifa Stars kutoka Ivory Coast baada ya kutolewa kwenye hatua ya Makundi.
"Inauma kutolewa mapema wakati wenzetu wanaendelea na mashindano, lakini ni kitu cha kawaida kwenye mpira lazima ukubaliane nacho. Sisi tumekubali na tupo tayari kuyafanyia kazi mapungufu yetu ili tukirejea tuwe bora zaidi.
"Mechi zote zilikuwa ngumu lakini mchezo wa kwanza (dhidi ya Morocco) ndiyo ulikuwa mchezo mgumu zaidi, kila mmoja anawajua Morocco ni timu bora sana, kwa hiyo tulipambana kwa uwezo wetu lakini hatukuweza kupata matokeo.
"Siri yangu kufanya vizuri ni kutokana na ari yangu ya kujituma uwanjani nikijua kwamba nalipambania Taifa langu. Nina haki ya kulipigania taifa langu popote, hicho ndicho kilikuwa kinanipa nguvu ya kuona kwamba nina deni kubwa kwa Watanzania wenzangu," amesema Bacca.