Unamkumbuka Bacary Sagna? Yule mwamba aliyetamba sana kwenye Ligi Kuu England akiwa na vikosi vya Arsenal na Manchester. Beki wa kulia huyo wa zamani wa Ufaransa ameibuka na kuweka bayana kile anachokiona kwenye mchakamchaka wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu.
Sagna alisema, Tottenham Hotspur hata wafanyeje hawawezi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu kwa sababu si washindani na muda wowote watalimwaga tu kama ilivyo kawaida yao.
Spurs kwa sasa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kukusanya pointi 20 katika mechi nane ilizocheza hadi sasa. Spurs katika mechi nane ilizocheza kwenye Ligi Kuu England hadi sasa, imeshinda mechi sita na kutoka sare mbili, ikiwa haijapoteza mchezo wowote, Lakini, Sagna alisema tena kwa msisitizo kikosi hicho cha kocha Ange Postecoglou hakina uwezo wa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Sagna alisema: “Mbio za ubingwa zitakuwa kati ya Arsenal na Manchester City kwa sababu Spurs wataboronga kama kawaida yao. Na hilo sisemi mimi tu kwa kuwa ni shabiki wa Arsenal. Sioni kabisa kama wataweza kulinda kiwango chao na kucheza kwenye ubora huo wa sasa msimu wote.“
“Ukimweka kando Heung-Min Son, sioni mchezaji mwingine yeyote kwenye kikosi hicho anayeweza kuongoza timu hiyo au kuipa nguvu kubwa Spurs kwenye mbio za ubingwa.”Hata hivyo, Sagna ana na aliongeza: “Arsenal wanaonekana walipata somo msimu uliopita na sasa watatuliza akili yao kwenye kukaba na kulinda matokeo wanayopata.”