Ni kweli siku hazigandi, lakini rekodi ya Abdi Kassim ‘Babi’ a.k.a Ballack wa Unguja inaendelea kuishi katika vichwa vya mashabiki wa soka nchini.
Ndio. Fundi huyo wa mpira aliyekuwa mahiri kwa kufumua mashuti makali uwanjani akiwatungua makipa, anaendelea kukumbukwa kutokana na rekodi aliyoiweka ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya ufunguzi wa uwanja huo, Taifa Stars ikiizamisha Uganda ‘The Cranes’ kwa bao 1-0 Septemba Mosi, 2007.
Mbali na rekodi hiyo, kiungo mshambuliaji huyo aliyetamba na klabu kadhaa nchini na nje ya Tanzania, bado anakumbukwa kwa makubwa aliyoyafanya enzi akicheza na Mwanaspoti lililokuwa katika michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika kwa shule (ASFC) 2024 lilifanya mahojiano maalumu naye.
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika wakati wa mashindano hayo yaliyofanyika mjini Unguja, Babi alifunguka mambo mengi ikiwamo kutoa baraka kwa kina Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama na nyota wengine wa kigeni kuendelea kukamua nchini akiamini watainua wazawa.
YEYE NA ADEBAYOR
Babi alipata bahati ya kutambuliwa na CAF kama lejendari wa soka la Tanzania kwa kukumbukwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao Kwa Mkapa.
Nyota huyo wa zamani aliungana na nyota wa zamani wa Arsenal, Manchester City, Real Madrid na timu ya taifa ya Togo, Emmanuel Adebayor, pamoja na mchezaji wa zamani wa Nigeria, Daniel Amokachi na nahodha wa zamani wa Banyana Banyana Amanda Dlamini ambao waliwafunda vijana mambo mbalimbali kuhusu soka na maisha baada ya kustaafu soka.
WANASOKA KUJITAMBUA
Akizungumza na wachezaji wa U-15 kutoka nchi mbalimbali walioshiriki michuano hiyo, Babi anasema ili waweze kufanikiwa inawapasa kujitambua na kufuata malengo yao pasipo kuyumbishwa na mtu yeyote kwani siri ya mafanikio katika soka ni kujitambua.
“Ili uweze kudumu katika soka inabidi uzingatie nidhamu na kujitambua kwanini unacheza hii itakufanya uweze kutimiza malengo yako uliyojiwekea pamoja na kufuata ushauri mzuri unaopewa na waliokutangulia na pia lazima kukumbuka kuwekeza kwani maisha ya soka ni mafupi sana usipojipanga utaishia kuwa mzigo kwa wenzako.”
PACOME, SAIDO FRESHI
Wadau mbalimbali walikuwa na maoni tofauti juu ya idadi ya mastaa wa kigeni kuwa 12, lakini kwa Babi yeye anaona freshi tu hao kina Aziz Ki, Pacome, Kipre Jr, Saido Ntibazonkiza, Clatous Chama na wengine waendelee kukamua kwani ni chachu kwa wazawa.
Babi anasema uwepo wa wachezaji 12 wa kigeni uwaamshe wazawa kujituma kwa bidii, kuhakikisha viwango vyao vinakuwa na nguvu uwanjani kama ilivyokuwa nyakati zao, japo idadi ya wageni ilikuwa ndogo, lakini wao hawakushtushwa na wageni zaidi ya kupambana ili kula nao sambamba na kuzibeba klabu walizozichezea.
“Kulikuwa na idadi ndogo ya wachezaji wa kigeni nyakati zetu, kama kina Kally Ongala, Moses Odhiambo, Benny Mwalala, Banza Tshikala na ulikuwa ukiangalia vikosi vya Simba na Yanga vilikuwa na wachezaji wenye vipaji na nidhamu.
Anaongeza: “Wazawa kama kina Haruna Moshi ‘Boban’, Mussa Mgosi, Amir Maftah,Said Maulid ‘SMG’, Nurdin Bakari, hapo ni nani wa kuwekwa nje? Ilifikia hatua wageni wenye-we walikuwa wanasubiri benchi.
“Kuna wakati mwingine najiuliza kwa nini Nurdin hakucheza nje ya nchi, alikuwa na kipaji kikubwa mno, tuliocheza naye tunajua, wakati wa mazoezi mnashawishika kumuangalia na kufurahia burudani yake.”
Mbali na hilo, Babi anasema kuna haja ya kuandaa vijana wengi ambao watakuwa wanacheza nje ya nchi, ambao watakuwa mbadala wa kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Abdi Banda, Himid Mao ambao kwa sasa wanaiwakilishi Tanzania huko walipo.
“Niwapongeze Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia na katibu wake Wilfred Kidau, wamekuwa mstari wa mbele kuandaa timu za vijana, ambao wakiwekewa misingi mizuri, tutapata profesheno wengi wanaocheza nje,” anasema.
Ombi lake kwa TFF, ni kuandaa kozi za viongozi wa klabu mbalimbali zinazohusu majukumu yao ya kisoka, jambo analoamini litasaidia kuepusha migogoro isiyo na maana.
“Nimecheza ndani na nje ya nchi, viongozi wa klabu wakipata elimu ya majukumu yao, yapo matatizo watayaepuka, kuna wakati wanasababisha baadhi ya vijana wawe na nidhamu mbovu, kwani wanashindwa jinsi ya kuishi nao.
Anaongeza: “Mfano mzuri ni kesi ambazo wachezaji wanazishitaki klabu FIFA, kama viongozi wakipata elimu watajua jinsi ya kuepukana na hayo mambo, ukiachana na hilo kozi za waamuzi ziwe zinafanywa mara kwa mara.
STARS MIAKA 16
Anasema tangu alipoanza kuzichezea timu za taifa kwa maana ya Taifa Stars na Zanzibar Heroes mwaka 1995-2011 sawa na miaka 16, kitu ambacho kilimbeba, ilikuwa nidhamu ndani na nje ya uwanja, kujituma na kuyafanyia kazi maelekezo ya makocha.
“Zamani kulikuwa na vipaji vikubwa, ukipata nafasi lazima uiheshimu, kwani unajua ukizingua mwingine anapewa na anaonyesha uwezo. Jambo jingine nilipenda kucheza soka kutoka moyoni.
Anaongeza: “Bao ambalo sitakaa nilisahau kati ya mengi niliyofunga nikiwa na Stars ni dhidi ya Uganda, dakika 90 zilimalizika kwa bao 1-0, kwanza Uwanja wa Benjamin Mkapa ulikuwa mpya, mashabiki walijitokeza kwa wingi, lilikuwa bao la ushindi, ilikuwa mwaka 2007.”
Kitu kinachomshangaza kwa wachezaji wa sasa, iwe kwenye klabu ama timu za taifa, wakionyesha uwezo kidogo na kuanza kutegemewa katika timu, basi wanaanza kutoa dharura za muda mwingi.
“Hakuna kitu kibaya ukigundua timu zinakutegemea, unaanza kuwasumbua viongozi ili mradi tu uonekane hakuna kama wewe, mambo kama hayo wanafanya wachezaji wasio na malengo na wanakuwa hawajui nini wanakitaka katika maisha yao,” anasema.
MASHUTI YA KUUA NYOKA
Wakati anacheza, mbali ya kuwa fundi wa boli, Babi alikuwa na nguvu za miguu. Alikuwa anatisha kwa kupiga mashuti makali kama anayeua nyoka na kufunga mabao ya mbali, ikiwemo kutoa asisti nyingi na anasimulia kilichokuwa nyuma ya hilo:
“Mazoezini nilikuwa mapiga mashuti 100 kila siku, nikichoka nilikuwa naishia mashuti 90, hiyo ilikuwa awepo kipa ama asiwepo, ndio maana nikiingia kwenye mechi nilikuwa napiga na kufunga mabao ya mbali, pia nilikuwa nafanya sana mazoezi ya kutoa asisti.
Anaongeza: “Kila kitu ukikifanya kwa moyo, lazima bidii itakuwepo, kuna wakati nawashangaa vijana wa sasa, wakicheza msimu mmoja kwa mafanikio, unaofuata viwango vyao vinakuwa vimeshuka.”
FEI TOTO, MUDATHIR
Anawazungumzia viungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ (Azam) na Mudathir Yahya (Yanga), wanavyomfuata na kuomba ushauri wa kitu gani wafanye ili kucheza kwa muda mrefu.
“Kwanza hao vijana wamelelewa kwenye malezi ya kidini, nidhamu na wakaleleka, kutokana na majina yao kuwa makubwa ingekuwa ngumu kunifuata na kuniomba ushauri, nimekuwa nikiwaelekeza baadhi ya mambo na ninawafuatilia wanachokifanya uwanjani.
Anaongeza: “Haijalishi kiatu cha ufungaji bora kimeenda kwa Stephane Aziz Ki, kwangu mimi mchezaji bora ni Fei Toto kwa sababu mabao 19 aliyoyafunga ni juhudi binafsi kazionyesha.”
KWA SASA ANAFANYA NINI
Babi amesomea ukocha ngazi ya Diploma B ya CAF, na ana mpango wa kwenda kusoma Diploma A, malengo yake ni kuwasaidia vijana kufikia ndoto zao za soka.
“Kuna vipaji vingi ambavyo vinahitaji kukuzwa kwenye misingi sahihi, nchi zilizoendelea ambazo wachezaji wake wengi wapo nje ya mataifa yao, ukifuatilia zilijenga misingi sahihi kwenye soka la vijana.
Anaongeza: Nashukuru jinsi ambavyo TFF na ZFF ambavyo zinaweka nguvu kwa vijana, huenda matokeo yake yanaweza yasionekane siku za usoni, ila vitakuwa na manufaa makubwa baadaye.”
MAFANIKIO YAKE
Anasema amejenga, ana biashara za kuuza vifaa vya michezo, maduka ya vyakula, vinavyomuingizia pesa za kujikimu.
”Ndio maana nasisitiza wachezaji kuiwaza kesho yao zaidi, wanaweza wakawa na majina makubwa, wakajikuta wanaishi maisha magumu baadaye.”
Mbali na hilo, anafurahishwa na uwepo wa Kombe la Muungano, ambalo analiona litakuwa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.
“Kombe la Mapinduzi linatoa fursa kubwa kwa wachezaji wa Zanzibar, kuonyesha uwezo wao, na Kombe la Muungano litazidi kuimarisha umoja na mshikamano kati ya watu wanaotoka Bara na Visiwani,” anasema.
KIKOSI CHAKE BORA
Omary Ally, Hilal Khalfan, Feisal Salum, Omary Juma, Moshi Shaaban, Said Muharami, Maalum Songoro, Rama Hamza, Mahmoud Hamza, Abdi Kassim, Ahmed Golo, kikosi hicho ni cha wachezaji wa zamani wa timu ya Mlandege wa Zanzibar kasoro Rama Hamza (Mtibwa).
“Kikosi hicho kilikuwa cha moto, kilichukua ubingwa wa Zanzibar mara saba, wachezaji walikuwa na vipaji vikubwa na nidhamu ya juu,” anasema.
TIMU ALIZOPITIA
2002-03 (Mlandege), 2004-06 (Mtibwa), 2007-10 (Yanga), 2011 (Long An FC), 2011-12 (Azam FC), 2013 (KMKM), 2014 (UTM F.C.), 2016-18 (Jang’ombe Boys), 2018-19 (Mawenzi Market), 2019-20 (KMKM).