Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Babacar ni Zulu mpya au Aucho wa Msimbazi?

 Babacar Sarr Dimba.jpeg Babacar Sarr.

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Yanga SC waliwahi kumsaini Mzambia aliyeitwa Justine Zulu. Rafiki yangu Hussein Omary niliyekuwa nae Ofisi za New Habari 2006 pale Sinza akampa jina la Mkata Umeme.

Mkata Umeme likaenda kuwa jina kubwa nchini kuliko lile la Zulu lililokuwa katika Hati yake ya Kusafiria ‘Passport’. Nje ya uwanja Zulu aliliuza jina lake. Ndani ya uwanja Zulu alikuwa mchezaji wa hovyo.

Dirisha lijalo Yanga SC wakamfungulia mlango ulioandikwa EXIT. Akaondoka nchini. Sidhani kama alijali sana. Aliondoka, huku Akaunti zake zikiwa zimenona. Maisha yanataka nini zaidi ya Pesa?

Baada ya muda mrefu kupita hatimaye Yanga SC wakarudi tena sokoni kumsajili Mganda. Alikuwa Khalid Aucho. Huyu hakuja na mbwebwe kama za Zulu, lakini ndani ya uwanja akaenda kuuwa msaada.

Miaka mitatu sasa tangu Yanga SC wamchukue Aucho, Simba SC wamelivamia soko na kumsajili Msenegal, Babacar Sarr. Huyu anafanana vitu vingi na kina Aucho, Zulu.

Babacar ni baba la milaba minne lenye misuli mikubwa tayari ni mchezaji wa Simba SC. Huyu ni kiungo halisi wa ulinzi kama ilivyokuwa kwa Aucho, Zulu. Matamanio ni mengi. Mashabiki wa Simba SC wanatamani kumuona zaidi Babacar.

Walimuona jana usiku pale Zanzibar katika pambano lao na Jamhuri pale Visiwani. Alicheza dakika 20 katika pambano lile. Lakini Simba SC hawajamsajili Babacar kwa ajili ya mechi zenye sura ya Jamhuri.

Amesajiliwa kwa ajili ya mechi za kiume dhidi ya kina Waydad, Al Ahly, TP Mazembe. Hizi ndiyo mechi zilizowafanya Simba SC watoke Dar es Salaam hadi Dakar kumsajili Babacar.

Ni mapema mno kusema lolote juu ya Babacar kwa sasa, licha ya wasifu wake kuonesha ni mchezaji mahiri. Nimeona picha yake inayotembea mitandaoni akiwa amesimama pembezoni ya Cristiano Ronaldo katika mechi, sio Mtaani wala Disko.

Sijali sana kuhusu picha ile ambayo manazi wa Simba SC wameigeuza fimbo ya kuwachapia watani zao Yanga SC. Katika yote kuanzia taifa alilotoka Babacar, picha yake na Ronaldo hadi wasifu wake kiujumla, naamini katika muda ndiyo nianze kumuhukumu.

Muda ndiyo hakimu mzuri. Kupitia muda tutajua Babacar ni mchezaji wa namna gani. Lakini kwa sasa ni mapema kuandika lolote lile linalomuhusu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live