Kama ilivyo kwa wazazi, huwa na mipango yao juu ya watoto wao, bila kujua kuwa baadae inaweza isitimie ndivyo ilivyotokea kwa Mzee Abdallah Hamad ‘Bacca’.
Kuna wakati unamwacha mtoto au mtu wako wa karibu kufanya kile anachokipenda zaidi hata kama wewe hukipendi kwa sababu yeye ndie anayekifanya.
Lakini tunaambiwa ni bora kumwacha mtu afanye anachokipenda zaidi kwani tunaamini atakifanya kwa moyo na juhudi.
Katika mahojiano maalumu na Baba wa Bacca akiwa visiwani Zanzibar, amefunguka mambo mengi sambamba na kuweka bayana asivyotaka mwanae kutua Msimbazi, hata kama itakuwa kufuata pesa.
Kwa nini hataki mwanae aende Simba? Endelea naye katika makala haya...!
ILIVYOKUWA
Baba Mzazi wa Ibrahimu Bacca anasema, wakati staa huyo alipokuwa mdogo alipenda mpira na yeye aliiona picha halisi ya maisha yake ya nyuma.
“Mimi nilipata ajira kupitia mpira wakati huo nacheza nafasi ya kipa namba moja wa Kidike FC iliyoko Pemba ambayo iko ligi daraja la pili.
Nikaenda Chuo cha Mafunzo na hapo ndipo nilipopata ajira moja kwa moja, wakati nacheza nafasi hiyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.”
KIPA HADI KIUNGO
“Katika maandalizi ya sherehe za Mapinduzi nilipata ajali nikaangukia mkono na kuumia vibaya.
Hapo ndipo nilipoacha kucheza kama kipa na kuingia ndani kuwa kiungo, lakini bado nilikuwa nafanya vizuri sana.”
MALEZI YA BACCA
Mzee Abdallah anasema; “Nilikuwa mkali sana kwa watoto, sikutaka ujinga maana hawa ukiwachekea watakupanda kichwani.
Ila pamoja na yote Bacca alikuwa mkorofi, sikumwelewa anataka nini mwanzoni maana shule hakutaka na alikuwa mtundu, hivyo nilivyojua anapenda nini nikamwambia mke wangu amwache afanye anachotaka.”
IMANI YAKE
Anasema; “Niliamini soka ni kazi kama zilivyo nyingine na limenipa nini kwa hiyo nikaamua kumpa tu Bacca uhuru.
Hata wazazi wengine kuna wakati wakubali tu kuwasikiliza watoto kile wanachopenda kufanya, ila viwe vitu vyema na sio viovu.
Niliwahi kutamani sana mwanangu acheze Yanga ijapo sikuweza kumwambia yeye wala mama yake.”
YANGA DAMU
Abdallah anasema kwake tangu zamani hakuwa na machuguo ya timu yoyote zaidi ya Yanga bila kujua nini kitakuja kutokea mbele.
“Nimeishabikia Yanga kwa kipindi kirefu sana, hivyo sikujua kama mwanangu atakuja kuichezea, pia hata Bacca naye alikuwa shabiki wa timu hiyo hiyo.”
MAOKOTO MAZITO
Anasema mpira ni kazi yenye kuingiza pesa kirahisi na ameziona kwa mtoto wake.
“Bacca kamaliza nyumba na pesa anayolipwa inaweza kutulipa mara tatu ya mshahara ambao tunaupata sisi wazee wake.”
SIKU ALIYOINGIA YANGA
Anaelezea furaha yake; “Wakati Bacca anachaguliwa Yanga nilifurahi na hivi sasa anavyoupiga mwingi basi navimba sana ninaposikia sifa zake.
Lakini ndoto zangu zimetimia kwani naipenda Yanga, hivyo alipochaguliwa nikajua tu atacheza huko kwani yuko vizuri.”
KOCHA WA KWANZA
“Mimi naujua mpira hivyo akizingua uwanjani mimi ndio wa kwanza kumkosoa na vipo vinavyoniudhi akiwa uwanjani.
“Nikiongea naye namwambiaga aache mchezo wa vurugu unaopelekea kupata kadi mara kadhaa,kwahiyo nakuwa mwalimu wake katika kila makosa anayoyafanya.
“Napenda kumwona ana nidhamu sio uwanjani tu hata katika maisha ya kawaida.”
SITAKI AENDE SIMBA
Anasema hatamani kumwona mtoto wake anaenda kuichezea Simba licha ya masuala ya kipato.
“Maombi yangu mwanangu asichezee timu pinzani, kwani watanipa wakati mgumu kama anaoupata mke wangu kwa sasa.”
USHAURI WA BABA
Anasema; ”Wakati mwingi naongeaga naye ili kumweka sawa, hasa mambo ya starehe, pia kufanya uwekezaji ili kama akistaafu mpira basi asiwe na maisha magumu.”
“Inawezekana asitake kuvaa gwanda tena maana hatujui mambo ya kesho, hata akiacha basi awe na uelekeo mzuri wa kimaisha baada ya Yanga au timu nyingine.”
DOGO NOMA
Anasema, “Mtoto wangu wa mwisho Mudhir Abdallah, ambaye ni mshambuliaji hodari ameanza kufahamika kwa kipaji chake na mimi namsapoti sana.”
Nitamkomalia mpaka afikie malengo kama nilivyofanya kwa Bacca na ni hatari huyu kuliko kaka yake, jambo linalonipa nguvu zaidi.”
MDOGO WAKE BACCA
Anaitwa Mudhir Abdallah, Mwanafunzi wa darasa la saba, akiwa ana malengo makubwa ya mpira, anazungumza na Mwanaspoti na kusema ya moyoni juu ya timu anayotaka kuichezea.
“Nikimaliza elimu ya juu ninatamani kucheza Yanga kama mshambuliaji kwani ni timu ninayoishabikia na kuipenda sana licha ya kuwa kaka yangu anaichezea.
Naipenda kwa mapenzi yangu binafsi sio ya baba, mama au kaka ndio maana naamini nitafika pale.”
AMKATAA MAMA
“Mama anataka nikachezee Azam lakini hiyo ni mipango yake, mimi sitaki hata kama wanatoa hela nyingi ila ninachotaka ni kucheza Yanga, pesa baadae.”
VYOTE VINASONGA
“Napata muda wa kusoma siku tano katika wiki ila ijumaa jioni naanza kucheza mpaka Jumapili ndio mwisho.
“Baba ndio amenipangia hiyo ratiba ili nisije kufeli kwani natakiwa kusoma kwa bidii ili nije kuwa mchezaji msomi.”
USHIKAJI
“Mimi na kaka sio marafiki sana akija namsalimia tu na ninaendelea na mambo mengine, labda nikiwa mkubwa huko ndio tutakuwa karibu na akiwa Dar basi naongea nae tu kwenye simu.”
KIBU NOMA
“Nampenda sana Kibu Denis kwa sababu anaujua mpira vizuri na ana mbinu za kuwaweza wapinzani.
Pia anacheza nafasi moja ninayoipenda na kuichezea, hata alipocheza na Yanga nilikuwa namhofia sana asije akafunga kwani anajua kupiga mashuti ya mbali.”