Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bab’kubwa! Ligi Bara inavyowabeba Wazenji

Feisal Salum Fei Toto'' Feisal Salum

Sat, 11 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Soka la Zanzibar mdogo mdogo, likizidi kukuwa kadiri siku zinavyokwenda huku kukiwa na mabadiliko yanaonekana hii ni kutokana na kutoa wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Bara (TPL) kwa kipindi hiki.

Katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15, mwaka huu, jumla ya wachezaji watano waliokuwa wakikipiga Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) walikwenda Bara na kufanya ifike idadi ya nyota 30 kutoka visiwani hapa wanaokipiga TPL.

Licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti ya wadau wakisema michuano ya Kombe la Mapinduzi ndio inayochangia wachezaji wengi kupata nafasi ya kwenda Bara na si vyinginevyo, ukweli ni kwamba Zanzibar ni moja ya eneo lenye vipaji vya soka kutokana na mfumo wake ulivyo.

Utamaduni wa Zanzibar kuibuka na kukuza vipaji tangu wadogo ni moja ya sababu inayowabeba wachezaji wa visiwani hapa, licha ya kuangushwa na kukosa stamina ukilinganisha na wale wa Bara wanaoonekana kuwa wagumu kwa aina ya lishe wanayopata na mazoezi yao pia.

Hata hivyo, wale wanaoamini Mapinduzi Cup ndio kama njia ya vipaji vya wachezaji wa visiwani humo kuokena, wanapingwa na baadhi ya wadau wakisema mchezaji hawezi kupafomu moja kwa moja kwenye michuano hiyo ya wiki mbili na yenye mechi chache isipokuwa ni Ligi Kuu ndio inayomjenga na kumpa fursa ya kupangwa kuchezwa kwenye michuano hiyo.

Wanaotetea hoja wanasema baada ya kucheza vizuri ligi kwani timu inakuwa na wachezaji wengi lakini wengine huishia benchi kutokana na viwango vyao.

Majembe matano mapya Wachezaji watano waliotoka kupitia dirisha dogo la usajili wote timu zao zilishiriki michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi 2023, huku Mabingwa wapya, Mlandege wakiongoza kwa kutoa wachezaji wengi (watatu).

Wachezaji hao ni kipa Yusuf Ali ‘Mpelule’ aliyechukua tuzo ya Kipa Bora, mshambuliaji Bashima Saul Saite na kiungo Abdulswamad Kassim ambao wote wamejiunga na Geita Gold.

KVZ nayo imetoa wachezaji wawili akiwamo kipa Ibrahim Abdalla ‘Parapanda’ (Singida Big Stars) na Michael Joseph Godlove aliyekuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo akitokea Simba ambaye ametimkia Namungo, huku akiwa amefunga mabao saba ya ZPL.

Mchezaji mwingine aliyesajiliwa dirisha dogo ni mshambuliaji Mohammed Mussa aliyekuwa kwa mabingwa wa zamani wa Tanzania, Malindi aliyetua Simba akiwa amefunga mabao saba kwenye ligi hiyo.

Mtazamo tofauti Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) linasema soka la visiwani linazidi kukua baada ya kuporomoka tangu ilipofutwa Ligi Kuu ya Muungano na kukosekana kwa wafadhili waliokuwa wakiwekeza kwenye klabu na kutoa ushindani wa kweli ndani na nje ya nchi.

Mtazamo wa kukua kwa soka la visiwani unatokana na idadi ya wachezaji wa Zanzibar wanaosajiliwa kwa mpigo kwenda Bara kuongezeka ikisema hufika sio chini ya watano na kuna wakati wanafikia saba wakitua klabu mbalimbali za Bara zikiwamo Simba, Yanga na Azam.

Katibu mkuu wa Shirikisho hilo, Hussein Ahmada Vuai alisema wanajivunia kuona vijana wao wanakwenda kucheza kwenye ligi ambayo ipo miongoni mwa ligi 10 bora barani Afrika .

“Tulikuwa na taarifa za wachezaji wengi ambao walitakiwa na timu za Bara lakini wengine walishindwa kukamilisha taaratibu za usajili kutokana na muda uliokuwepo, wale ambao tumewapa vibali kwenda kucheza huko ni wachezaji watano,” alisema.

Anasema wanaamini kucheza Bara watapelekea kuitangaza Ligi ya Zanzibar lakini na wao kujiongezea vipato vyao ingawa amedai baadhi ya wachezaji hushindwa kumudu changamoto za Ligi ya Bara na kurudi Zanzibar.

Sebo, Fei wakomaa

Ukiachana na Abdallah Kheri ‘Sebo’ wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mudathir Yahya Abas, Abdalla Shaibu ‘Ninja’ Yanga na wengineo ambao wamedumu kwa kipindi kirefu kucheza Bara, lakini wapo baadhi hucheza msimu mmoja na wengine nusu msimu tu.

Wapo wachezaji ambao hawakudumu Ligi ya Bara kama Majid Khamis ‘Dudu’ (Kagera Sugar 2020) sasa hivi anacheza KVZ, Abraham Othman na Abdalla Mundhir wote walicheza Singida United nusu msimu tu kwa sasa Othman anaichezea KMKM, Omar Haji ‘Chareli’ alitoka Mlandege kwenda Namungo FC sasa KMKM, Iddi Farjala, Hassan Banzu nao waliamua kurudi nyumbani.

Hii inatokana na ligi hiyo kuwa ngumu zaidi pia mchanganyiko wa wachezaji kutoka mataifa tofauti nayo inasababisha wachezaji hao kutokuwa na viwango vizuri wakiwa huko tofauti na hapa Zanzibar ambapo ligi haina wachezaji wengi wa kigeni.

Akizungumza Chareli anasema shida kubwa wanayoipata wakiwa huko ni kutopata namba kwenye timu ambazo wanasajiliwa na hivyo inakuwa ngumu wao kubakia kwenye klabu hizo.

“Tatizo kubwa tunakuwa hatupati namba tunakaa benchi na kama huchezi basi hakuna timu ambayo itakuona ndio maana tunakuwa tunaondoka na tunarudi tena nyumbani kujipanga upya.

“Mimi mwenyewe nilikaa msimu mzima Namungo FC sijacheza mechi hata moja nafanya mazoezi na wenzangu vizuri tu lakini siku ya mechi naishia kwenye mbao, kwaiyo haina haja ya kubaki kwa sababu sisi tunataka tucheze tuonekane kama tutakaa benchi kila siku hatutajitangaza,” alisema Chareli.

ZFF kiroho safi ZFF inasema inafahamu changamoto hiyo ipo kwa wachezaji wengi ambao wanashindwa kufanya vizuri wakisajiliwa Bara kutafuta njia mbadala ili kuona vitu hivyo havijirudii mara kwa mara.

Vuai anasema sasa wanajaribu kuwaelekeza wachezaji wao na mawakala wao jinsi gani Ligi ya Bara ilivyo lakini pia tofauti ya uendeshaji wa klabu za hapa Zanzibar na Bara na kwamba kinachowaathiri zaidi ni mazingira ya hapa Zanzibar na huko.

“Timu za Bara zikisajili wachezaji wa Zanzibar wanawasajili kwa sababu ya uwezo wao, shida iliyopo ni mazingira wanayokwenda kukutana nayo wakiwa huko ndio inapelekea wasidumu kwenye klabu hizo na kuamua kurudi hapa,” alibainisha Vuai. Miaka ya nyuma Zanzibar iliwahi kusajili wachezaji kutoka Bara na hata nje ya nchi.

Chanzo: Mwanaspoti