Baada ya kukusanya pointi sita kwenye uwanja wa nyumbani, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Fikiri Elias amevutiwa na morali na kasi ya mastaa ambao amewapa mapumziko ya siku tatu kupisha mechi za Kombe la Shirikisho la Azam (FA).
Coastal Union imepata pointi sita baada ya kuichapa Mbeya City bao 1-0 na Tanzania Prisons 1-0 michezo yote ikicheza Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Akizungumza kocha huyo alisema: “Matokeo mazuri tuliyoyapata ni moja ya chachu ya mafanikio. Kama kocha tangu nimepewa timu nimekutana na wachezaji wakiwa na morali nzuri tuna wiki mbili mbele kabla ya mchezo wetu na Singida Big Stars.”
“Nimetoa siku tatu za mapumziko kwa wachezaji wangu baada ya kazi nzuri waliyoifanya kwa kukusanya pointi sita nyumbani sasa watarudi kambini Jumatano tayari kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya SBS Machi 12 sisi ndio tutakuwa wenyeji wa mchezo.”
Alisema mapumziko aliyotoa anaamini hayataathiri ubora wa wachezaji wake ambao wamemuonyesha kuhitaji matokeo kwenye kila mchezo ulio mbele yao ili kujitengenezea mazingira mazuri kwenye msimamo wakihakikisha hawashuki wala kucheza (mtoano) playof.
Huu ni ushindi wa pili kwa kocha Fikiri tangu aanze kukaa kwenye benchi la Wagosi wa Kaya, ambapo alishinda 1-0 dhidi ya Mbeya City na jana akaichapa Prisons pia 1-0.
Kibarua kingine kigumu alichonacho Fikiri ni mchezo wa marudiano dhidi ya Singida Big Star utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Vita (Mkwakwani), ambapo katika mchezaji wa kwanza Coastal Union FC walishinda kwa bao 2-1 mjini Singida.