Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baada ya mziki wa Azam leo, balaa linakuja Simba

Robertinho X Bocco Kocha wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akiteta na Nahodha John Bocco

Sun, 7 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' amesema dhamira yake ya kushinda mechi ya leo Jumapili dhidi ya Azam FC katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ni moja tu ya mikakati yake mizito ya kuifanyia makubwa timu hiyo, lakini kwanza atahitaji kukiimarisha kikosi chake ikiwamo kupitisha panga kwa wachezaji ambao hawajaingia katika mfumo wake.

Robertinho ameiongoza Simba kufika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na akiiwezesha kuwafunga mahasimu wao Yanga baada ya kushindwa kuwatambia katika Ligi Kuu Bara kwa muda mrefu.

Na wakati anajiandaa kuikabili Azam FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, kocha huyo raia wa Brazil anajiandaa kufanya uamuzi mgumu mwishoni mwa msimu huu kwa baadhi ya mastaa wa Simba kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kizuri kama walivyotabiriwa licha ya majina yao makubwa.

Hili linakuja siku chache baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Mei 3 kwenye Uwanja wa Majaliwa ambao Robertinho aliwapa nafasi wachezaji wengi ambao huwa hawaanzishi katika kikosi chake cha kwanza na wengi wao kucheza kwa kiwango ambacho hakikumfurahisha Mbrazil huyo.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya timu hiyo zinasema licha ya mabadiliko ya kikosi katika mchezo uliopita na Namungo, Robertinho alitumia fursa kupeleka ujumbe kwa viongozi akihitaji kusajiliwa wachezaji wengine wazuri wenye uwezo zaidi ya waliopo.

Robertinho inaelezwa hakufurahishwa na baadhi ya wachezaji waliocheza mchezo huo ingawa hakuwa na jinsi ya kufanya mabadiliko hayo kwa sababu wengi wao wa kikosi cha kwanza walikuwa na kadi za njano hivyo angehatarisha uwepo wao katika mechi dhidi ya Azam leo.

"Wachezaji wote ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kocha ameahidi kuwapa nafasi ya kucheza kwenye mechi zote tatu zilizobaki na ameanza na Namungo ugenini sasa imebaki mechi tatu ila hadi sasa kocha hajafurahishwa na kiwango cha baadhi yao;

"Amesema viongozi watakuwa wameona ni kwanini amekuwa akiwatumia wachezaji wale wale na kuacha wengine wakikaa benchi kwa sababu viwango vyao vinaachwa mbali sana na wanaopata nafasi ya kucheza hivyo anahitaji kitu kifanyike ili timu iweze kuwa na wachezaji ambao watakuwa wanapeana changamotom" kilisema chanzo cha ndani kutoka Simba.

Chanzo hizo ambacho hakikutaka kutajwa kiliongeza:

"Kwa asilimia kubwa amekiri kuwa wachezaji waliopata nafasi ya kucheza mchezo dhidi ya Namungo wamemuangusha hivyo wamemfanya aendelee na msimamo wa kuwaamini wanaopata nafasi ya kucheza huku akisisitiza kuna michezo ambayo anakosa wachezaji wa kuwapumzisha baadhi yao kutokana na kukosa ubora anaoutaka akitolea mfano eneo la ushambuliaji."

Nyota wanaoweza kuondoka mwishoni mwa msimu huu ni Nelson Okwa na Victor Akpan walioko Ihefu kwa mkopo, Augustine Okrah, Mohamed Ouattara, Ismail Sawadogo, Nassoro Kapama, Habib Kyombo, Beno Kakolanya, Jonas Mkude na Gadiel Michael.

Mastaa kama Pape Sakho na Moses Phiri licha ya kutegemewa kutokana na ubora wao ila ni miongoni mwa wanaotajwa pia kutaka kuondoka kutokana na kutokuwa na furaha tangu Robertinho alipoingia ndani ya kikosi hicho Januari 3, mwaka huu.

Mechi tatu zitakazoamua hatma ya mastaa hao ni dhidi ya Ruvu Shooting ambayo itapangiwa tarehe, Polisi Tanzania (Mei 24) na mchezo wa mwisho wa kuhitimisha msimu huu wa 2022/23 dhidi ya Coastal Union Mei 28, ambayo yote Simba itacheza nyumbani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live