Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu baada ya kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara.
Ahmed amesema anafahamu wanasimba wanapitia maumivu makali baada ya kushushiwa mvua ya magoli lakini anawasihi kutokutoka kwenye malengo kwani bado wana michezo mingine.
“Kwenye Mkutano wa wanahabari nilisema, hii ni mechi ambayo matokeo yake hua yanaacha furaha ya kudumu au huacha maumivu ya kudumu kwenye mioyo ya mashabiki wake isivyo bahati ni sisi ndo tunabaki na maumivu ya kudumu” ameandika Ahmed na kuongeza,
“Kila Mwana Simba anawaza sababu tofauti tofauti iliyosababisha tupoteze mchezo wa jana, iko namna sahihi ya kujua sababu hizo nayo ni utulivu tuwape Viongozi, Benchi la Ufundi na Wachezaji wetu utulivu wa kujitathmini kwa maslahi ya mechi zijazo”.
Meneja huyo amemaliza kwa kusema Novemba 9 Simba ina mchezo dhidi ya Namungo hivyo ni vema wakajikita zaidi kuangalia alama tatu za mchezo huo.