Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baada ya Robertinho kuleta msaidizi wake, Simba yatoa tamko kuhusu Mgunda na Matola

Mgunda Nkoma Matola Mgunda na Matola

Sat, 21 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kutokana na ujio wa Kocha Msaidizi mpya wa Simba, Ouanane Sellami, kutoka  Tunisia, uongozi wa klabu hiyo umesema makocha wake wengine, Juma Mgunda na Selemani Matola, bado wataendelea kusalia katika kikosi hicho kilichotinga hatua ya makundi katika michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika,

Akizungumza nasi jijini jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah 'Try Again', alisema uongozi umeleta kocha mwingine ili kuimarisha benchi la ufundi na wanaamini uamuzi huo utaongeza ufanisi.

Try Again alisema walihitaji kuona benchi la ufundi la Simba linakuwa na nguvu na uwezo wa kukamilisha majukumu yake vizuri na huo ndio 'ukubwa' na si vinginevyo.

"Licha ya kuboresha kikosi, sehemu nyingine ya muhimu ni benchi la ufundi, tumemleta Ouanane kama kocha msaizidi yakiwa ni mapendekezo ya kocha mkuu. Makocha wote waliokuwepo wataendelea kubakia, tulichofanya ni kuongeza nguvu," alisema Try Again.

Naye Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema huo ni mwendelezo wa maboresho ya benchi la ufundi kama ilivyokuwa kwa timu zilizoendelea za Afrika Kaskazini au barani Ulaya.

"Ni mwendelezo wa maboresho ya benchi la ufundi, ukienda kwa wenzetu walioendelea unakutana timu ina makocha mpaka 10, na watu wengine zaidi wa benchi la ufundi, kila kocha ana eneo lake la kufundisha na kulifanyia kazi. Kuna makocha wa viungo, mabeki, washambuliaji, fiziki, makipa, watu wa vyakula, saikolojia, yaani kila eneo lina mtu wake na huko ndiko tunakoelekea, Simba hatuwezi kuwa na kocha mmoja tu kama Mungu, " alisema Ahmed.

Aliongeza kikosi chao kitaendelea kuwa na wataalam wengi kwa ajili ya kujiongezea maarifa kwa sababu malengo yao makubwa ni kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Ili ufike huko lazima ukusanye watu (makocha) wengi waje kukufanyia kazi," alisema Ahmed.

Aliongeza kikosi chao kiliondoka Dar es Salaam jana jioni na kuelekea Dodoma kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara Dodoma Jiji FC itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini humo.

"Tumesafiri na wachezaji wote, hadi wapya waliosajiliwa hivi majuzi wamejumuishwa katika safari hiyo, kasoro wanne tu na wameachwa kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya majeruhi ambao ni Mosses Phiri, Henock Inonga, Israel Mwenda na Peter Banda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live