Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limezifungia klabu za Kitayosce iliyoko Ligi Kuu Soka Tanzania Bara na Fountain Gate inayocheza Ligi ya Championship kufanya usajili katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya 2023/24.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mapema leo Jumatano (Julai 12) na Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ imeeleza kuwa, maamuzi ya FIFA ya kuzifungia klabu hiyo yamekuja, kufuatia Kocha Ahmed El Faramawy Yousef Mostafa Soliman kushinda kesi za madai dhidi ya klabu hizo.
Kocha huyo raia wa Misri ambaye alizifundisha timu hizo kwa nyakati tofauti alifungua kesi FIFA akipinga kuvunjiwa mikataba kinyume cha taratibu.
Baada ya Soliman kushinda kesi, klabu hizo zilitakiwa ziwe zimemlipa ndani ya siku 45 tangu uamuzi huo ulipotolewa, lakini hazikutekeleza hukumu hizo.
Wakati FIFA imezifungia klabu hizo kufanya uhamisho wa wachezaji kimataifa, Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limezifungia kufanya uhamisho wa ndani.
TFF imezitaka klabu kuheshimu mikataba ambayo zimeingia na wachezaji pamoja na makocha ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo kufungiwa kusajili.
“Iwapo klabu inataka kuvunja mkataba na mchezaji au kocha, inatakiwa kufanya hivyo kwa kuzingatia taratibu.” Imeeleza sehemu ya taarifa ya TFF