Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BATIGOL: Nilifunga 'hat-trick' nikakimbia na mpira, Simba dozi

Batgolllll Nilifunga 'hat-trick' nikakimbia na mpira, Simba dozi

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Miongoni mwa mastaa wakongwe nchini wanaokumbukwa ndani ya Simba na soka la Bongo kwa ujumla ni Emmanuel Gabriel ‘Batigol’ ambaye kwasasa ni meneja wa timu ya Fountain Gate inayoshiriki Ligi ya Championship.

Batigol kama mashabiki wa soka walivyokuwa wakimuita kutokana na umahiri wake wa kufunga mabao wakimfananisha na straika wa zamani wa Argentina, Gabriel Batistuta ‘Batigol’, aliifunga Yanga atakavyo pale walipokuwa wakikutana.

Staa huyu anafahamika na mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na ubora wake enzi hizo anacheza soka la ushindani akiwa miongoni mwa nyota wa kikosi kilichoiwezesha Simba kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati huo ikijulikana kama Klabu Bingwa Afrika na si hayo tu bali aliisadia kutwaa mataji mbalimbali yakiwemo ya Ligi na mengine waliyoshiriki.

Ndani ya Simba kulikuwa na kundi lililoitwa ‘East Coast’ ambalo lilikusanya wachezaji wengi kutoka Dar es Salaam kama Athuman Machupa, Shaban Kisiga, Sudi Abdi, Yahya Akilimali, Said Sued, marehemu Christopher Alex, Prince Kasonzo na Boniface Pawasa, hawa ni wale waliokuwa wakidaiwa kuwa kama wakongwe kwenye timu hiyo hivyo kuwa na nguvu kuliko wengine.

Kundi jingine lilikuwa ni la wanyonge na lilikuwa na wachezaji kama Juma Kaseja, Emmanuel Gabriel, Musa Hassan Mgosi, Nico Nyagawa, Nurdin Bakari, Dan Mrwanda, Kelvin Mhagama, Amri Said, Victor Costa huku Ulimboka Mwakingwe yeye akiitwa bosi kwa maana alikuwa katikati ya makundi hayo mawili.

Hivi karibuni Mwanaspoti ilifanya mahojiano na Batigol akaelezea baadhi ya mambo ambayo mashabiki hawajawahi kuyasikia kutoka kwake na kama wameyasikia basi ni kwa kusimuliwa ila yeye ameyaweka wazi.

ASEPA NA MPIRA WA HAT-TRICK

Anasema kuwa katika maisha yake ya mpira amewahi kufunga hat-trick nyingi lakini hakuwahi kupewa mpira anapofunga.

“Hata sikuelewa kwanini walikuwa hawanipi mpira nikifunga hat-trick, niliwahi kufunga hizo zaidi ya mara tatu, nilikuwa nasikitika tu lakini kuna siku pale Uwanja wa Uhuru niliona isiwe tabu wao si hawataki kunipa mpira nilifanya uamuzi mgumu kwa kumfuata kijana muokota mipira ‘Ball Boys’ baada ya mechi.

“Nilimwambia tu hebu nipe huo mpira, akanipa basi nikaenda nao kwenye chumba cha kubadilishia nguo, kelele zilianza huku mabosi wa TFF (FAT wakati huo) walianza kunitishia kuwa watanifungia, sitaki kuwataja majina isije ikaleta shida kwa kujengeana uhasama.

“Niligoma kurudisha na nilikuwa tayari kwa lolote lakini mabosi wangu wa Simba kipindi hicho walikuwepo kina Kasim Dewji ‘KD’ walinifuata na kuniambia nirudishe watanipa pesa nikanunue mpira, kweli kiongozi mmoja hapo hapo alitoa Sh60,000 na kunipa, mambo yakaisha,” anasema Batigol.

ANYIMWA ZAWADI YA MFUNGAJI BORA

Aliingia Simba msimu wa 2000/2001, ikiwa ni mara yake ya kwanza kucheza Ligi Kuu Bara na hapa anasimulia zaidi.

“Ilikuwa ndio ligi yangu ya kwanza kucheza, nikawa mfungaji bora nikifunga mabao 19 wakati huo timu zilikuwa ni 30, hata hivyo, TFF ilisema ligi hiyo inakwenda kuchezwa Sita Bora kwa timu sita zilizokuwa zimefanya vizuri ili apatikane bingwa.

“Tulicheza, Simba ikachukua ubingwa huku mimi nikiwa mfungaji bora pia kwani nilifunga mabao sita, lakini cha ajabu sikupewa zawadi na sikuambiwa sababu yoyote ile, hivyo ni matukio ambayo kwa mwingine yanaweza kumkatisha tamaa ila sikuwahi kukata tamaa,” anasema.

ISHU YAKE NA ABDALLAH JUMA

Abdallah Juma alikuwa straika wa Mtibwa Sugar, mwaka 2006 ndiye aliyeibuka mfungaji bora akimaliza ligi akiwa ametupia mabao 20. Batigol anafafanua juu ya Abdallah kuwa mfungaji bora.

“Ni kitendo ambacho pia kinaniuma hadi sasa, maana hakustahili kutwaa tuzo hiyo, mabao yake yaliyohesabika ni pamoja na yale waliyokuwa wanampa wachezaji wenzake waliofunga akiwemo Monja Liseki.

“Nilistahili niwe mfungaji bora maana Abdallah hadi anatangazwa alikuwa amenizidi bao moja, sasa baadaye siri ikatoka kwamba hakufikisha mabao hayo. Siri waliitoa wachezaji wenzake baada ya kuwatosa mgao aliopewa hivyo walikasirikia kitendo hicho.

“Zamani mpira ulikuwa hauonyeshwi kama hivi sasa, wachezaji walikuwa wakifunga wanaenda kushangilia kwenye kona na mwamuzi ‘anawauliza nani kafunga’ wanamtaja Abdallah kwasababu walikuwa wameutengeneza huo mpango na mwamuzi aliamini hivyo.

“Ila ajabu ni kwamba Abdallah mabao yake mengi alifunga kwenye Uwanja wa Manungu tu, kwanini kwingine alishindwa kufunga, na huu mjadala ulijadiliwa sana na vyombo vya habari ingawa sasa huwezi kubadilisha matokeo yaliyotangazwa,” anasema Batigol.

SIMBA DOZI

Kama kuna anayelikumbuka hili jina basi ni wale wa enzi zile lakini wengi wao hawafahamu kama miaka ya nyuma wachezaji wa Simba waliipachika jina jipya timu yao iliitwa Simba Dozi kutokana namna ilivyokuwa ikifanya vizuri.

“Kwanza kulikuwa na ushirikiano mkubwa kwa wachezaji, pale mbele tulikuwa mafowadi kama sita na wote tulicheza na kufunga, Athuman Machupa alianza kuingia Simba lakini wakati mimi nasajiliwa alikuwa ameenda nje kucheza ingawa baadaye alirejea na kunikuta.

“Nilicheza na wachezaji wote pale mbele akiwemo Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ naye alifunga sana ile ilikuwa Simba ya moto mwaka 2003, ndiyo maana tuliita Simba Dozi, mpinzani akija vibaya basi ajiandae kupigwa.”

Hata hivyo, anasimulia namna ambavyo vita yake ilivyokuwa na Machupa; “Machupa aliporejea kuna mambo yalitokea ila ni mambo binafsi, hivyo hata ufanyaji kazi uwanjani tukianza pamoja haukuwa mzuri, ndipo nilipowaeleza mabosi wangu kuwa nataka nianze kucheza na Mussa Hassan ‘Mgosi’.

“Au kama Machupa anaanza mimi niingie baadaye, au nianze yeye aingie baadaye, nashukuru viongozi walielewa nikaanza kucheza na Mgosi na alifanya vizuri maana alikuwa mchezaji wa jukwaani kutokana na kutopata nafasi.

“Nakumbuka kuanza kucheza na Mgosi ilikuwa kwenye mashindano ya Tusker, maana nilikuwa sipewi pasi na Machupa lakini yote hayo yalikuwa ni nyakati hizo na sina tatizo na naye kwasasa, maana wote hatupo tena kwenye mpira.”

ATUNZA MAMILIONI NYUMBANI

Anasema wakati anaingia kucheza Simba hakuwahi kufungua akaunti ya benki bali pesa zake zote alizozipata alizihifadhi nyumbani.

“Naweza kusema kwamba pesa nyingi nilizopata Simba kipindi kile nasajiliwa nilizitunza nyumbani tu, hata zile tulizokuwa tunapewa wakati wa mechi kama bonasi tunaposhinda nilizihifadhi nyumbani na sio benki. Wakati mwingine tulipewa hadi Sh300,000 timu ikishinda kwenye hizi mechi kubwa. Kwa wakati huo zilikuwa ni pesa nyingi.

“Ilikuwa ikifika kiasi fulani basi naenda kufanya jambo langu naanza kuhifadhi tena, na pesa hiyo ndiyo nilinunua hata kiwanja cha kujenga nyumba yangu Kitunda, sikutaka usumbufu wa kwenda benki niliona nyumbani ni mahali salama kwangu kwani mimi sio mtu wa starehe, sinywi pombe wala sivuti sigara, napenda muziki, hivyo pesa zilikuwa salama tu.”

KWA ZAMALEK HATUKULAMBA KITU

“Wengi wanahisi mwaka 2003 tulipowatoa Zamalek kwenye michuano ya CAF tulipata pesa nyingi sana, ila haikuwa hivyo, tuliahidiwa kila mtu kupewa Sh5 milioni lakini hatukupewa na waliopewa ni baadhi tu ambao walikuwa watu wao na ilikuwa pesa kidogo sana.

“Binafsi mafanikio hayo yalikuwa ni ya timu ila kwa wachezaji hatukuambulia kitu, hilo pia halikunikatisha tamaa kwani nilitimiza majukumu yangu.”

FAMILIA

Ana watoto watano ingawa ameachana na mke wake; “Haya ni maisha binafsi na kila mmoja ni namna anavyoona inafaa kuishi, mke wangu hakuwa mtu wa mpira kabisa, nilipomuoa ndipo alianza kuuelewa mpira hivyo hakuwa miongoni mwa wanaoshabikia mpira ila kwasasa hatuishi pamoja kwa maana ya kwamba tumeachana, kuna mambo tulitofautiana tu.

“Nilizaa naye watoto watatu, ila wengine ni wa mama mwingine, kwani sasa hivi kuna mtoto ambaye ni wa tano ambaye amezaliwa siku za hivi karibuni ni mchanga anaitwa Luis jina la mchezaji wa zamani wa Liverpool maana mimi ni shabiki wa timu hiyo.

“Huyu Luis mama yake bado hatujafunga ndoa na ninawapenda sana wanangu wote, mengi yalitokea kwenye ndoa yangu ya awali ila nashukuru Mungu nimesimama upya na maisha yanaendelea, ni mengi hutokea kwenye familia ila Mungu husimama nasi ndio jambo kubwa la kushukuru. Sasa nipo kwenye maisha mapya.” anasema Batigol.

NGASSA HAJANIZIDI

Winga wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Ngassa ndiye mfungaji bora wa muda wote wa Stars akiwa amefunga mabao 25 kwa kipindi chote alichoichezea timu hiyo, lakini Batigol anapingana na hilo akidai kwamba awali TFF walikuwa hawatunzi kumbukumbu kwani kuna waliomtangulia Ngassa wamefunga mabao zaidi ya hayo.

“Ngassa alikuwa mchezaji mzuri sana, sidhani kama anaweza kunishinda kwenye mabao ya Stars, nilifunga mabao mengi tangu nianze kuichezea tatizo kumbukumbu zetu wachezaji wa zamani zilikuwa hazitunzwi TFF hilo ndo tatizo, na wangekuwa wanasema amefunga kuanzia kipindi chake na siyo kwa wakati wote, wanatukosea adabu.

“Nakumbuka kuna mechi moja nilifunga mabao manne chini ya kocha Boniface Mkwasa na marehemu Mziray, 2001 nilifunga zaidi ya mabao tisa, wakati wa Maximo napo nimefunga mengi tu, sasa huwa najiuliza hizi rekodi huwa wanazitoa wapi, maana ni kutukosea wachezaji wa zamani na kutuvunjia heshima.

“Kikubwa TFF wanapotaka kutoa rekodi zao kwenye mambo kama haya wanapaswa kushirikisha baadhi ya watu miaka ya nyuma pengine huwa wanachukua rekodi za hivi karibuni tu.”

SIMBA vs YANGA

“Kwa zaidi ya miaka 9 au 10 niliyocheza Simba nimefungwa na Yanga mara moja tu siku ya ufunguzi wa Uwanja wa Mkapa, Yanga ilishinda bao 1-0, lakini kipindi chote tuliwafunga Yanga, na niliwafunga hata mabao mawili ingawa nasikitika nilishindwa kufikia rekodi ya kocha Abdallah Kibadeni aliyepiga hat-trick kwa watani katika ushindi wa mabao 6-0.

“Kibadeni anastahili kuheshimiwa na mastraika wote nikiwemo mimi, namheshimu sana ingawa kwa kipindi chote nilichocheza Simba nilifikia mabao zaidi ya 100, maana nilifunga mabao mengi sana.

“Upinzani wetu wa kipindi hicho ulikuwa ni mkubwa mno ukilinganisha na sasa hivi, awali timu moja ikifungwa basi hata mtaani huwezi kukatisha kwani mashabiki na wanachama inakuwa vurugu mno, ni moja ya mechi ambayo inakuwa ngumu mno hadi sasa hivi, kwani tuhuma za rushwa zinatokea wengine wanaweza hata kufukuzwa kikosini.”

Chanzo: Mwanaspoti