Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

BALAA ZITO! EPL yaingiza vichwa 14 Ballon d’Or 2021

Montage BallondOr2021 BALAA ZITO! EPL yaingiza vichwa 14 Ballon d’Or 2021

Mon, 11 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

PARIS, UFARANSA. MAMBO ni moto. Mastaa wa Ligi Kuu England wametawala kwenye orodha ya wanaochuana kuwania tuzo ya Ballon d’Or wakikaribia nusu ya wakali wote 30 wa awali waliotajwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mabingwa wa Ulaya, Chelsea na wa Ligi Kuu England, Manchester City kila moja imeingiza mastaa watano kati ya wanasoka 14 wanaokipiga Ligi Kuu England, huku wawili wakitokea Manchester United na mmoja mmoja Liverpool na Tottenham.

Mastaa wa Chelsea, Cesar Azpilicueta, N’Golo Kante, Romelu Lukaku, Mason Mount na Jorginho – moja ya timu inayopewa nafasi staa wake mmoja kushinda tuzo hiyo.

Man City wamewaingiza kwenye kinyang’anyiro Kevin de Bruyne, Ruben Dias, Phil Foden, Riyad Mahrez na Raheem Sterling.

Masupastaa wawili wa Kireno, Cristiano Ronaldo na Bruno Fernandes ndio watakaoiwakilisha Man United kwenye tuzo hizo, wakati Liverpool imemwingiza Mohamed Salah na Spurs inabebwa na Harry Kane kukamilisha orodha ya wakali 14 wa Ligi Kuu England waliongia kwenye kuwania tuzo ya Ballon d’Or kati ya wachezaji 30.

Kipa wa Chelsea, Edouard Mendy, yule wa Man City, Ederson na nahodha wa Leicester City, Kasper Schmeichel watachuana jino kwa jino kuwania tuzo ya Yacine Trophy inayoshirikisha makipa waliofanya vizuri mwaka husika.

Mason Greenwood wa Man United na Bukayo Saka wa Arsenal watachuana kuwania Kopa Trophy inayohusu wachezaji makinda, huku staa wa England na Borussia Dortmund, Jude Bellingham yupo kwenye kinyang’anuyiro hicho. Tuzo ya Ballon d’Or imekuwa ikitolewa kila mwaka, lakini mwaka wa jana iliahirishwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Supastaa wa Paris Saint-Germain, Lionel Messi, ambaye alishinda mara ya mwisho mwaka 2019 na kumfanya awe amefikisha idadi ya tuzo sita, anapewa nafasi kubwa ya kubeba tena mwaka huu.

Miamba hiyo ya Ufaransa, PSG imeingiza mastaa wanne ambapo sambamba na Messi wengine ni kipa Gianluigi Donnarumma na washambuliaji Neymar na Kylian Mbappe.

Wachezaji wawili wa Inter Milan, Nicolas Barella na Lautaro Martinez, mabeki wa kati wa Juventus, Leonardo Bonucci na Giorgio Chiellini na yule wa AC Milan, Simon Kjaer wataiwakilisha Serie A kwenye tuzo hizo.

LaLiga imeingiza wachezaji watano, wawili kutoka Real Madrid ambao ni Karim Benzema na Luka Modric, huku Villareal ambao ni mabingwa wa Europa League wameingiza kwenye mchakato Gerard Moreno, Barcelona imemwingiza kinda Pedri na mabingwa wa La Liga, Atletico Madrid ni Luis Suarez.

Straika wa Bayern Munich, Robert Lewandowski na wa Borussia Dortmund, Erling Haaland ni wakali wawili wa kutoka kwenye Bundesliga watakaochuana kwenye tuzo hiyo ya ubora kabisa kwenye mchezo wa soka duniani.

Orodha ya mastaa 30 watakaochuana tuzo ya Ballon d’Or 2021.

Cesar Azpilicueta (Chelsea), Nicolo Barella (Inter), Karim Benzema (Real Madrid), Leonardo Bonucci (Juventus), Giorgio Chiellini (Juventus), Kevin De Bruyne (Man City), Ruben Dias (Man City), Gianluigi Donnarumma (AC Milan, PSG), Bruno Fernandes (Man Utd), Phil Foden (Man City), Erling Haaland (Borussia Dortmund), Jorginho (Chelsea), Harry Kane (Tottenham), N’Golo Kante (Chelsea), Simon Kjaer (AC Milan), Robert Lewandowski (Bayern Munich), Romelu Lukaku (Inter, Chelsea), Riyad Mahrez (Man City), Lautaro Martinez (Inter), Kylian Mbappe (PSG), Lionel Messi (Barcelona, PSG), Luka Modric (Real Madrid), Gerard Moreno (Villarreal), Mason Mount (Chelsea), Pedri (Barcelona), Neymar (PSG), Cristiano Ronaldo (Juventus, Man Utd), Mohamed Salah (Liverpool), Raheem Sterling (Man City), Luis Suarez (Atletico Madrid).

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz